Dar es Salaam. Mwili wa Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya umewasili nyumbani kwake, Upanga, Dar es Salaam ambako utahifadhiwa hadi kesho Mei 11, 2025 utakapoagwa katika viwanja vya Karimjee.
Shughuli hiyo ya kuupokea mwili imefanyika leo Mei 10, 2025 ikiongozwa na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa na kushuhudiwa na waombolezaji mbalimbali waliofika msibani kutoa pole kwa familia.
Msuya aliyewahi pia kuwa makamu wa kwanza wa Rais, alifariki dunia Jumatano Mei 7, 2025 katika Hospitali ya Mzena iliyopo Kijitonyama, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa kijijini kwake, Usangi, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Mei 13, 2025.

Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi iliyofolewa jana, mwili wa Msuya utaagwa kitaifa katika Uwanja wa Karimjee, Jumapili ya Mei 11, 2025 na baada ya shughuli ambayo Rais Samia Suluhu Hassan atashiriki, utasafirishwa kwenda kijijini kwake Usangi, ambako shughuli za maziko zitafanyika.
Shughuli hiyo ya kuaga, katika viwanja wa Karimjee itafanyika kuanzia saa 3 asubuhi na kuongozwa na viongozi wa dini na kutolewa kwa salamu mbalimbali za viongozi.
Leo, maombolezo yakiwa yanaendelea nyumbani kwake hapo, waombolezaji waliupokea mwili huo uliowasilishwa saa 10:20 jioni ukiwa katika gari la Jeshi la Wananchi (JWTZ) na ukiwa umefunikwa bendera ya Tanzania.

Hatua za kuingiza mwili huo ndani zilichukua takribani dakika 20 ambapo familia ilikabidhiwa rasmi kwa ajili ya taratibu zingine za kifamilia na kufanyika kwa sala ya kuuombea.
Baadhi ya viongozi waliojitokeza katika hafla ya kuupokea mwili huo ni pamoja na Balozi Peter Ulanga, Mbunge wa Same, David Mathayo, Mbunge wa Mwanga na Mbunge Mwanga, Joseph Tadayo.
Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa ambaye pia ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa, Richard Kasesela na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Jordan Rugimbana.