Mwili uliokuwa ukigombaniwa na familia mbili wazikwa kwa mara ya pili

Simanjiro. Hatimaye mwili wa Jackson Joseph (29) uliokuwa ukigombaniwa na familia mbili, umezikwa leo Novemba 11, 2024 kwa mara ya pili katika makaburi ya familia yaliyopo Kijiji cha Msitu wa Tembo, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.

Jackson alifariki dunia Juni 16, mwaka huu na mwili wake kuchukuliwa na familia ya Richard Shoo (31) na kuzikwa Juni 25, mwaka huu katika kijiji cha Kibosho Kindi, ikidai ni mwili wa kijana wao Richard.

Baadaye familia ya Jackson iliibuka na kudai mwili huo ni wa kijana wao, ikaenda mahakamani ambayo iliamuru mwili ufukuliwe kwa ajili ya vipimo vya vina saba (DNA) kuondoa utata uligubika kwenye familia hizo mbili.

Septemba 4, mwaka huu, mwili huo ulifukuliwa kwa ajili ya kupimwa DNA na baada ya siku 57 kupita, Novemba mosi mwaka huu, majibu yalitoka kuwa mwili huo ni wa Jackson Joseph, hivyo kuiacha familia ya Shoo na maswali kijana wao Richard waliyeambiwa amefariki dunia na kuchukua mwili kuuzika yuko wapi.

Leo Jumatatu, Novemba 11, 2024 mwili huo umezikwa Msitu wa Tembo, huku padri kiongozi wa Parokia teule ya Msitu wa Tembo, Dismas Mtenga akiiasa jamii kuzingatia malezi bora kwa watoto ili kuzalisha viongozi wazuri wa baadaye.

Amesema ni jujumu la wazazi kuhakikisha wanawalea watoto wao katika misingi bora ya maadili na kuhakikisha wanakuwa waadilifu na waaminifu, hatua itakayowezesha kupatikana kwa viongozi bora wa familia na hata jamii.

“Kama mzazi hujamfundisha mtoto kuchagua pumba na mchele atakapotoka na kukutana na makundi mabaya kitakachotokea unakijua, malezi na makuzi ya kimaadili na utu ni muhimu, hivi vitatusaidia kwenye maisha.”

Aidha, ametumia pia nafasi hiyo kuwataka vijana kuzingatia maadili na kuhakikisha wanaweka akiba kila wakati, ili kujiletea maendeleo na kujitengenezea maisha bora ya baadaye.

Lusinde Paulo, rafiki wa marehemu enzi za uhai wake, amesema amempoteza rafiki mwema mwenye upendo na aliyependa kusaidia wenzake kila alipohitajika.

“Marehemu alikuwa rafiki  yangu, tumekuwa pamoja na tumecheza naye na tumeishi kama ndugu na mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa Juni 14, mwaka huu, lakini Juni 16 niliambiwa amefariki dunia. Alikuwa mtu wa upendo na alipenda kuishi kwa amani na kusaidia watu, nimempoteza rafiki ambaye alinisaidia kwa mambo mengi,” amesema Paulo.

Ilivyokuwa

Baada ya Jackson kufariki dunia Juni 16, mwaka huu, mwili wake ulichukuliwa na familia ya Richard Shoo na walidai ni wa kijana wao Richard na baada ya taratibu zote waliuzika kijiji cha Kibosho Kindi Juni 25, mwaka huu.

Hata hivyo, baada ya siku kadhaa kupita, familia ya Jackson iliibuka na kudai kuwa mwili uliozikwa ni wa kijana wao aliyeuawa Juni 16, 2024, hali iliyoibua sintofahamu kwa familia hizo mbili.

Septemba mosi mwaka huu, Polisi  wakiongozwa na mkuu wa upelelezi wilaya ya Moshi, wakiambatana na madaktari wawili, walifika katika familia ya Shoo kwa ajili ya kufukua mwili huo, lakini ilishindikana baada ya familia kudai kutoshirikishwa na kutaka kuonyeshwa kibali cha mahakama cha kufukua mwili ambacho polisi hawakwenda nacho wakidai wamekiacha ofisini.

Mwonekano wa kaburi kabla wa kufukuliwa huko mwili  ulikokuwa umezikwa na familia ya Shoo, Dungi, kibosho kindi Mkoani Kilimanjaro.

Hivyo, waliwaomba wenzao ofisini wakipige picha kisha wakitume kwa njia ya simu, lakini familia ilikataa na kudai wanahitaji kukiona hali ambayo ilifanya kuahirishwa kwa ufukuaji huo.

Septemba 4, 2024, familia zote mbili zilifika mahakamani na amri ikatolewa kwa mara nyingine kuwa kaburi likafukuliwe ili mwili huo utolewe na kupimwa DNA, kujiridhisha ni wa nani.

Baada ya kaburi hilo kufukuliwa, polisi waliondoka na jeneza lenye mwili na kwenda kulihifadhi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC ambako ulihifadhiwa na Novemba mosi majibu ya DNA yalitoka, hivyo kuiacha familia ya Shoo ikiendekea kuhaha kumsaka kijana wao, Richard Shoo.