
Dar es Salaam. Msanii maarufu wa fani ya uigizaji Joyce Mbaga (32) maarufu Nicole Berry na mwenzake Rehema Mahanyu (31) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Washtakwa hao wamepandishwa kizimbani mahakamani hapo, leo, Jumatatu, Machi 10, 2025 na kusomewa mashtaka matatu na Wakili wa Serikali Rhoda Maingu.
Akiwasomea mashtaka hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira, Wakili Rhoda amesema washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Julai 2024 na Machi 2025 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika shtaka la kwanza washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kuongoza genge la uhalifu kwa lengo la kujipatia fedha.
Wakili Rhoda amedai washtakiwa walitenda kosa hilo kwa lengo la kujipatia faida kwa kupokea amana au miamala kutoka kwa jamii bila kupata leseni kutoka Benki Kuu (BoT).
Katika shtaka la pili washtakiwa wote wanatuhumiwa kuwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025 wakiwa eneo lisilofahamika ndani ya mkoa wa Dar es Salaam walipokea amana ya Sh185.51 milioni kutoka kwa jamii bila kuwa na leseni.
Wakili Rhoda amedai katika shtaka la tatu washtakiwa waliendesha mfumo wa malipo bila kuwa na leseni ya malipo inayotolewa na BoT.
Hata hivo, baada ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Rugemalira aliwaeleza kwamba hawatakiwi kujibu chochote hadi pale upelelezi utakapokamilika na Mahakama hiyo inayoketi Kinondoni kupewa kibali cha kusikiliza kesi hiyo, ndipo watakapojibu kama ni kweli au si kweli.
Wakili Rhoda ameieleza Mahakama kwamba upelelezi bado haujakamilika na kwamba hawana pingamizi ya dhamana ya mshtakiwa.
Wakili Jeremiah Mtobesya anayemtetea Nicole na Avelina Nelson anayemtetea Rehema wameiomba Mahakama itoe dhamana kwa wateja wao kwa sababu mashtaka wanayoshtakiwa nayo yanadhaminika.
Hakimu Rugemalira amekubaliana na hoja na maombi hayo na akawataka kuwasilisha mahakamani fedha taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya kiasi cha fedha wanazodaiwa kukusanya kutoka kwa umma, kama moja ya masharti ya dhamana yao kwa utaratibu wa kugawana kiasi hicho.
‘Kesi yenu ina dhamana, lakini katika kosa la pili la kupokea miamala kutoka kwa jamii mlipokea Sh185,515,000, sheria inaruhusu washtakiwa kugawana nusu ya fedha hii kwa ajili dhamana,” amesema Hakimu Rugemalira na kuongeza:
“Nusu ya fedha hii ni Sh92, 757, 500. Hivyo kila mmoja wenu atatakiwa kuwasilisha mahakamani fedha taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh46,378,750,” amesema.
Pia, Hakimu Rugemalira amewataka kuwa na wadhamini wawili kila mmoja, wenye barua za utambulisho kutoka Serikali za Mitaa na kama ni muajiriwa awasilishe barua ya ofisi yake.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 24, 2025 washtakiwa na wamerudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana.