Mwigizaji Nicole mbaroni akidaiwa kutapeli mamilioni

Dar es Salaam. Mwigizaji na mfanyabiashara, Joy Mbaga maarufu ‘Nicole Berry’ anashikiliwa na jeshi la polisi Dar es Salaam kwa tuhuma za kujipatia zaidi ya Sh100 milioni kwa njia za udanganyifu.

Akizungumza na Mwananchi leo Machi 5, 2025, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Nicole (32) alikamatwa Machi 3, 2025 akielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kusafiri kwenda Lagos nchini Nigeria.

“Anatuhumiwa kujipatia pesa kwa njia mbalimbali za udanganyifu, kwa kutengeneza magrupu ya upatu kwenye mitandao kinyume na sheria. Anatengeneza watu wa uongo wa kwenye magrupu hayo, anawavuta watu.

“Wakati mwingine wakiweka laki moja baada ya mzunguko anakuonesha watu pengine 48 kwa hiyo wewe unaweza kuwa wa kwanza, wa tatu au wa kumi kupokea.

“Kwa hiyo ukipiga hesabu unaona baada ya muda mfupi unaweza kupata kama milioni nne na kitu. Anatengeneza magrupu mengi tu, watu wanachangia lakini matokeo yake ni magrupu ambayo siyo ya ukweli, yana watu wengi ambao siyo wa ukweli. Wewe unayeingia ndiyo unakuwa unatapeliwa,” amesema Muliro.
 

Amesema hadi sasa kuna walalamikaji zaidi ya 18 ambao wamejitokeza kwenye Kituo cha Polisi cha Oysterbay. 

“Zaidi ya Sh100 milioni za watu zimechukuliwa katika mfumo wa udanganyifu. Watu mbalimbali wanazidi kufika kituoni wakidai na wenyewe wamechukuliwa pesa zao. Mpaka sasa yupo Kituo cha Polisi cha Oysterbay. 

“Wito wangu ni watu kuwa watulivu wanapotaka kufanya biashara zozote ambazo zinapitia njia hii ya mtandao, hasa magrupu ya upatu. Unaingia na hauna uhakika kwa hiyo watu tumekuwa tukiwatahadharisha mara kadhaa kutofanya biashara ya aina hiyo,” amemalizia Muliro.

Wanachosema wanasheria

Kutokana na tuhuma hizo, kumekuwa na maoni tofauti tofauti kutoka kwa wanasheria kuhusiana na adhabu anayoweza kupatiwa mwigizaji huyo endapo atapatikana na hatia.

Akizungumza kuhusiana na tukio hilo, mwanasheria, John Mallya amesema kuchezesha upatu ni kosa kisheria.

“Kosa la upataji fedha kwa njia ya udanganyifu limezungumzwa kwamba adhabu yake ni miaka saba jela na hakuna ‘option’ ya faini. Lakini kuna vifungu ambavyo vinaweza kuruhusu faini ikalipishwa kwa maana mazingira ambayo kosa lilitendeka,” amesema Mallya.

Mbali na John, naye wakili Fulgence Massawe amesema kucheza na kuchezesha upatu vyote ni kosa kisheria.

“Kwa sababu bado polisi wanafanya uchunguzi ni vigumu kusema amefanya kosa gani. Labda angekuwa amesomewa mashtaka mahakamani, lakini sisi tunavyojua kwa Tanzania ni kosa la jinai kuendesha upatu. Siyo kuendesha tu hata kushiriki.

“Ndiyo maana hata wanaodai hela ya upatu inakuwa vigumu kwenda kushtaki kwa sababu hata wao wanakuwa ni waalifu. Mwisho wa siku itaishia kwenye makosa ya upatu na uhujumu uchumi, adhabu zake ni miaka 20 au 30 lakini kwa sasa kusema yeye adhabu yake ni ipi ni mpaka polisi wafanyie kazi,” amesema Massawe.