Seoul, Korea Kusini. Tasnia ya filamu na burudani Korea Kusini imepata pigo baada ya taarifa za kifo cha mwigizaji maarufu Kim Sae-ron (24) aliyefariki dunia nyumbani kwake jijini Seoul.
Kwa mujibu wa vyombo vya usalama nchini humo, mwili wa msanii huyo uligunduliwa na rafiki yake jana Jumapili Februari 16, 2025 na kutoa taarifa Polisi.

Polisi wamesema kuwa uchunguzi wa awali haujaonyesha dalili za uhalifu, lakini wanaendelea kuchunguza mazingira ya kifo chake.
Maisha na kazi
Kim alizaliwa Julai 31, 2000, na alianza safari yake ya sanaa akiwa na umri wa miaka tisa kupitia filamu A Brand New Life (2009), ambayo ilimpatia umaarufu mkubwa.
Aidha aliendelea kung’ara zaidi kupitia filamu The Man from Nowhere (2010), ambayo ilimfanya kuwa miongoni mwa waigizaji chipukizi wenye mvuto mkubwa katika tasnia ya filamu ya Korea Kusini.
Katika miaka iliyofuata, alishiriki katika filamu zingine kubwa kama ‘A Girl at My Door’ (2014) na tamthilia za televisheni zikiwemo ‘Secret Healer na Leverage’.

Mnamo 2023, alirejea kwa kishindo kupitia mfululizo wa filamu katika mtandao wa Netflix ikiwemo Bloodhounds, iliyopokewa vizuri na watazamaji.
Hata hivyo, maisha yake ya sanaa yaligubikwa na matatizo binafsi ambapo mwaka 2022, alikumbwa na kashfa ya kuendesha gari akiwa amelewa, ambapo alisababisha uharibifu wa mali jijini Seoul.
Tukio hilo lilisababisha kupigwa faini ya Won milioni 20 (Sh35.8 milioni) na kumsababishia changamoto kubwa za kisaikolojia na kijamii, hali iliyomfanya apunguze shughuli zake za kisanii.

Mwaka 2024, Kim alitangaza kurejea katika sanaa kupitia kipindi cha Dongchimi kinachorushwa na Korea Kusin TV, lakini alijiondoa dakika za mwisho kutokana na matatizo ya afya na msukosuko wa maoni hasi kutoka kwa mashabiki.
Kifo chake kimezua mjadala mpana kuhusu shinikizo linalowakabili wasanii wa Korea Kusini, hasa katika tasnia inayojulikana kwa ushindani mkali na matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa baada ya taratibu za mazishi kukamilika huku familia na mashabiki wakiendelea kuomboleza msiba huo mzito.
Imeandikwa na Evagrey Vitalis kwa msaada wa Mashirika.