Mwenyekiti wa Kamati ya UN: Vita vya Israel Ghaza vinaturejesha ‘zama za ushenzi usio na udhibiti’

Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa ya Kuchunguza Mienendo ya Israel Palestina (SCIIP) amesema, vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza vinairejesha nyuma dunia hadi kwenye zama za ushenzi usio na udhibiti.

Peter Mohan Maithri Pieris ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha rasmi ripoti ya Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa ya Kuchunguza Mienendo ya Israel huko Palestina, ambayo imefananisha sera ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza na Mauaji ya Kimbari.

Pieris, ambaye pia ni balozi wa Sri Lanka katika Umoja wa Mataifa amezihutubu nchi wanachama katika makao makuu ya umoja huo mjini New York, akisema: “ninapowasilisha ripoti hii, ninawasihi kila mmoja wenu, msijifanye sikio la kufa; historia haitasahau kwa tulivyoamua kutochukua hatua na tunavyoshiriki (katika mauaji)”.

Peter Mohan Maithri Pieris

Mwenyekiti wa SCIIP amefafanua kwa kusema: “mbele ya macho yetu, tunaruhusuu kurejea kwenye zama za ushenzi usio na udhibiti”.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Pieris amezihutubu nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa akisema: “yale mateso tuliyoapa kuwa hayatatokea tena, sasa yameruhusiwa chini ya kivuli cha usahihi wa kiteknolojia, uchezeaji wa kiujanja wa sheria za kimataifa na upotoshaji wa habari “.

Aidha, amekumbusha kuwa kutochukua hatua Jamii ya Kimataifa kuhusiana na yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza sio tu kunamaanisha kushindwa kulinda maisha ya watu wasio na hatia kutokana na uharibifu wa vita, lakini pia ni kuufuta mfumo wenyewe wa kimataifa wa sheria.

Utawala haramu wa Kizayuni unaendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ghaza kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, huku ukiungwa mkono kikamilifu na kwa kila hali na madola kadhaa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, Ujerumani na Uingereza.

Wapalestina wasiopungua 43,922 wameuawa shahidi hadi sasa na wengine zaidi ya 103,898 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto katika vita hivyo vilivyoanza Oktoba 7, 2023…/