
Siha. Mwenyekiti wa Baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha) Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Elizabeth Mollel amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean Road, iliyopo Jijini Dar es salaam.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Siha, Imma Saro amesema kiongozi huyo amefariki alasiri Aprili 18, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean Road.
“Kwa masikitiko makubwa, natangaza kifo cha Mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Siha, Elizabeth Mollel, kilichotokea Aprili 18, 2025 saa 9 alasiri katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu,” amesema mwenyekiti huyo.
Amesema kifo chake ni pigo kwa chama hicho kwa kuwa alikuwa ni kiongozi mchapakazi, mpambanaji na aliyekuwa akijituma katika kazi.
“Kifo cha Elizabeth ni pigo kwa chama, tumepoteza mpambanaji. Nilifahamu Elizabeth Mwaka 2010 wakati wa uchaguzi mkuu akiwa anajitolea katika chama, amelea wengi amefanya makubwa ndani ya chama na alikuwa ni kiongozi asiyechoka kukipenda chama,” amesema Sarro.
Aidha amasema chama hicho, kitatoa taarifa zaidi baadaye kuhusu maziko ya kiongozi huyo.
“Niwape pole wanachadema wote na wananchi wote wa Wilaya ya Siha kwa msiba huu mzito,” amesema Sarro.
Akizungumzia kifo cha kiongozi huyo, mjumbe wa mkutano mkuu wa Chadema Taifa, Lameck Mmary amesema kifo cha kiongozi huyo ni pigo kwa chama hicho kwa kuwa alikuwa ni kiongozi mwenye msimamo na jasiri.
“Marehemu Elizabeth alikuwa mwenzetu katika uongozi, alikuwa mwanamke jasiri sana licha ya mazingira magumu ya kisiasa na hakuwahi kurudi nyuma katika upambanaji wake, hakika tumepoteza kiongozi mahiri sana katika Wilaya yetu,” amesema Lameck.
Amesema, “Wakati akiwa diwani wa viti maalumu mwaka 2015 alisimama kidete kukipigania chama hata wakati wenzake wakiunga juhudi kwenda CCM yeye ni mwanamke pekee aliyeweza kusimama mpaka alipomaliza kipindi chake mwaka 2020.”
Katibu wa Bawacha Wilaya ya Siha, Fransisca Mmary amesema wamepoteza kiongozi msikivu, mshauri mzuri na aliyekuwa na maono makubwa kuhusu maendeleo ya wanawake.
“Bawacha Wilaya ya Siha, tumepokea kwa majonzi makubwa kifo cha kiongozi mwenzetu, tumeumia sana, alikuwa ni dada mwema, alikuwa msikivu na mshauri mwema na alikuwa na maono makubwa kuhusu wanawake,” amesema katibu huyo.
Mmoja wa wananchi wa wilaya hiyo, Namorita amesema kiongozi huyo alikuwa ni mama mpambanaji na aliyeweza kusimama na kukema, kusema ukweli kwa maslahi mapana ya wananachi wa wilaya hiyo.
Elizabeth wakati wa uhai wake alikuwa Mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Siha kwa nyakati tofauti tangu mwaka 2014 hadi 2025 na amewahi kuwa diwani viti maalumu mwaka 2015 hadi 2020, na mjumbe wa Serikali ya Kijiji Ngarenairobi kwa miaka 15.