Mwenyekiti Soka la Wanawake Mbeya afariki dunia

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Soka la Wanawake Mkoa wa Mbeya (MWFA), Atupakisye Jabir, amefariki dunia leo Aprili 3, 2025 wakati akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Atupakisye ameongoza chama hicho kwa takribani miezi tisa huku akiwa kiongozi wa kwanza wa nafasi hiyo kikatiba na kuacha historia ya kusimamia vyema soka la wanawake Mbeya.

Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (Mrefa), Lucas Kubaja amethibitisha kifo cha kiongozi huyo akieleza kuwa ni simanzi na pigo kumpoteza mdau huyo mkubwa katika mpira wa miguu.

Amesema pamoja na kuongoza muda mfupi kwenye nafasi hiyo, lakini atakumbukwa kwa mengi katika kuandaa na kusimamia misingi ya soka kwa wanawake.

“Huko nyuma hatukuwa na uongozi rasmi, hivyo yeye ndiye mwenyekiti wa kwanza katika kuongoza soka la wanawake Mbeya, alikuwa mpambanaji sana, tumempoteza mdau mkubwa katika mpira wetu.

“Amefariki leo, taarifa zisizo rasmi mwili unatarajia kufika Mbeya kesho na kuagwa kwa ajili ya mazishi huko Busokelo, lakini tunasubiri taratibu zaidi za familia, alikuwa mtumishi wa serikali,” amesema Kubaja.

Kwa upande wa Mjumbe wa Soka la Wanawake, Elisia Mwaipopo amesema walikuwa na ushirikiano mzuri na mkubwa na marehemu Atupakisye akieleza taarifa za kifo chake zimewashtua sana.

“Ni pigo kubwa katika soka la wanawake Mbeya, alikuwa mstari wa mbele kusukuma maendeleo na kushawishi mpira na michezo kwa ujumla,” amesema Elisia.

Mmoja wa wadau wa soka jijini Mbeya, Tefa Mwandalila amesema marehemu Atupakisye atakumbukwa kwa mengi katika mageuzi ya soka la wanawake na kwamba alikuwa na mipango mingi ya kukuza, kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto wa kike.

“Hatujajua kama malengo yamefikia kwakuwa hata kwenye uchaguzi mwaka jana aliahidi kusimamia mpira wa wanawake uchezwe, tunamuombea awe na pumziko jema,” amesema Mwandalila.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *