Wakuu wa nchi na serikali wa mataifa mbalimbali barani Afrika kuanzia Alhamis ya wiki hii watawasili jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, kushiriki kwenye mkutano muhimu wa 38 wa Umoja wa Afrika, kujadili masuala mbalimbali na kumchagua Mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja huo siku ya Jumamosi.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Kuanzia uwanja wa ndege wa Addis Abbaba Bole, unaanza kukutana na mabango yanayonadi kikao hicho
Kabla uchaguzi wa uenyekiti wa tume ya AU na naibu wake siku ya Jumamosi,mawaziri na wakuu wa taasisi tofauti chini ya AU watakuwa wanakongamana kutoa ripoti ya mwaka ,maswala ya usalama mdogo na migogoro kwenye ukanda yakitazamiwa kushamiri.
Marais wote pia watakuwa wanahutubia kongamano hilo kabla uchaguzi.
Na katika shughuli ambayo imevutia bara zima ni kinyanganyiro cha uenyekiti kati ya nchi ya Kenya ikiwakilishwa na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, Djibouti ikiwakilishwa na Mahamoud Ali Youssouf huku mgombea wa tatu akiwa ni Richard Randriamandrato kutoka madagascar.

Waziri wa mambo ya nje nchini Kenya Musalia Mudavadi ameshawasili Addis huku Raila akitazamiwa alhamisi baada ya kampeni za lala salama katika nchi ya Burundi na Somalia.
Kinyanganyiro kingine pia kinatazamiwa kushuhudiwa katika uchaguzi wa naibu mwenyekiti wa tume hiyo ya AU ambapo mataifa mawili ya Afrika Kaskazini ,Morocco na Algeria ambayo hayana uhusiano mwema zinakutana kwenye debe.

AU ina nchi wanachama 55 ambazo zinatazamiwa kushiriki kura hizo ,ila kuna mataifa sita ya Burkina Faso, Gabon, Guinea, Mali, Niger na Sudan ambazo uanachama wao ulisitishwa kutokana na mizozo ,hivyo hawana ruksha kushiriki.