Mwenyekiti Kamati ya Maadili TFF azungumzia sakata la Ali Kamwe, Mazanzala

HUKO mtaani hadi mtandaoni, gumzo ni taarifa zilizovuja mapema Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amepewa kibano kwa kufungiwa kutokana na kukutwa na hatia ya kutoa maneno ya kejeli kwa waamuzi, hata hivyo kwa mujibu wa kanuni zilizopo kibano cha Kamwe kinaweza kuwa tofauti.

Ipo hivi. Kamwe aliburuzwa mbele ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho ya Soka Tanzania (TFF) kwa kosa la kuchapisha andiko katika mitandao ya kijamii, akitoa maoni juu ya waamuzi na kutaka mamlaka kuingilia kati kwa kutoa kauli.

Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya Ligi Namba 46: Udhibiti wa Viongozi kifungu cha 10 kinachoeleza; ‘Ni marufuku kwa kocha/kiongozi wa timu/klabu kushutumu au kutoa matamshi/maandiko/picha/video kwa lengo la kumkejeli au kumshutumu au kumkashifu au kumdhalilisha mwamuzi yoyote wa mchezo/kiongozi wa TFF/FA (M)/TPLB kwenye vyombo vya habari na mahali pengine popote.’

Kanuni hiyo ina ainisha adhabu kwa anayeikiuka kwa kusomeka; ‘Kiongozi atakayekiuka atafungiwa idadi ya michezo isiyopungua mitatu au kipindi kati ya miezi mitatu (3) mpaka kumi na miwili (12) na/au faini kati ya shilingi laki tano (500,000/-) na milioni mbili (2,000,000).’

Andiko hilo la Kamwe alilichapishwa katika akaunti ya Instagram Februari 3, 2025 akionyesha wasiwasi wake na ubinadamu wa makosa ya waamuzi kwenye mechi za ligi kuu ikiwa ni makosa kwa mujibu wa kanuni kabla ya Februari 12, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi iliwapeleka Kamati ya Maadili ya TFF akiwa sambamba na Ofisa Habari wa Kagera Sugar, Hamis Mazanzala kwa tuhuma za kutenda makosa ya kimaadili katika machapisho yao kwenye kurasa za mtandao wa Instagram.

Baada ya wawili hao kufika Kamati ya Maadili walisikilizwa utetezi wao na sasa inaelezwa wanachosubiri ni hukumu baada ya kusikiliza mashtaka yao, lakini ghafla tangu juzi usiku ndipo taarifa zisizo rasmi zimesambaa wawili hao wamefungiwa miaka miwili. Muda huo uliotajwa ni kinyume na kanuni iliyopo kama ilivyoainishwa hapo juu.

Mwanaspoti lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF, Wakili Kichere Mwita Waissaka, ili kupata ukweli wa jambo hilo na alisema kwa kifupi watatoa taarifa rasmi juu ya sakata hilo, kwani bado hawajatoa hukumu kama inavyoelezwa mitandaoni.

“Siwezi kuzungumzia habari za mitandaoni hao wanaotoa taarifa sio watu sahihi kama hukumu ingekuwa imetolewa ungeona taarifa kutoka kwa Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo huyo ndiye mtu sahihi wa kuzungumzia hilo mara baada ya kamati kutoa hukumu.”

Licha ya majibu ya mwenyekiti huyo, lakini Mwanaspoti limedokezwa, hukumu hiyo imeshatolewa na mamlaka zimeamua kukausha ili kupisha kwanza Dabi ya Kariakoo ipigwe Machi 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kisha ndipo kila kitu kiwekwe hadharani, ingawa haijafahamika muda halisi walioadhibiwa maofisa habari hao wa Yanga na Kagera.