
Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amekemea vikali vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na watu wanaodai kuwa na uwezo wa kusamehe madeni ya kodi.
Onyo hilo linakuja kufuatia kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa watuhumiwa wawili wanaodaiwa kufanya udanganyifu kuwa wao ni maofisa wa TRA na kuwa wanao uwezo wa kusamehe madeni ya kodi.
Mwenda ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 6, 2025 jijini Dar es Salaam.
Amesema hakuna mtu yeyote, hata watumishi wa TRA, mwenye uwezo wa kisheria kufuta madeni ya kodi badala yake yatafutika kwa kulipwa.
Kamishna Mwenda amesema kuwa madai ya kufuta madeni ya kodi ni uongo na utapeli, na amewaonya wananchi na walipakodi kutoamini watu wanaodai kuwa na uwezo huo.
“Mtu anayedai kuwa anaweza kufuta deni la kodi anafanya udanganyifu na ni kosa la kisheria, sheria za Usimamizi wa Kodi zinatoa ruhusa ya kusamehe riba na adhabu kwa masharti maalumu, lakini si kufuta kodi halali,” amesema Kamishna Mwenda.
Katika taarifa hiyo, Kamishna Mwenda ameeleza kuwa kifungu cha 70 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015, kama ilivyorekebishwa, kinampa Kamishna Mkuu mamlaka ya kusamehe riba na adhabu kwa masharti yaliyowekwa na kwa upande wa ushuru wa forodha, kifungu cha 249 cha Sheria ya Usimamizi wa Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pia kinampa Kamishna Mkuu mamlaka ya kusamehe riba na adhabu.
“Mamlaka ya Mapato Tanzania itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaodai kufuta madeni ya kodi kwa lengo la kuiba walipakodi,” amesema Mwenda.