
Dar es Salaam. Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) limetaja vikwazo vitatu wanavyokumbana navyo watu wenye ulemavu wanaposaka ajira, huku mtandao uwezeshaji wa wenye ulemavu mahali pa kazi ukitajwa ni mwarobaini wa changamoto za ajira kwa kundi hilo.
Vikwazo vinavyotajwa kuwakumba wenye ulemavu wanaposaka fursa za ajira ni mtazamo na mazingira.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Machi 11, 2025 na Mkurugenzi ILO kwa Ukanda wa Afrika Mashariki, Caroline Mugalla katika hafla ya uzinduzi wa Mtandao wa Kitaifa wa Watu Wenye Ulemavu katika maeneo ya kazi (NBDN) iliyoandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE).
Caroline amesema mtandao huo unalenga kuwajengea uwezo wanawake na wanaume wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika fursa za uwezeshaji kiuchumi, kuboresha uelewa na kuwajengea ujasiri waajiri sekta binafsi ili kutengeneza mazingira jumuishi mahali pa kazi.
“Ili kukabiliana na changamoto wanazopitia wenye ulemavu ILO imeanzisha Mtandao wa Walemavu kwa taasisi za biashara duniani ili kuongoza kampuni za kimataifa zinazofanya kazi na ILO kutetea ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye kampuni na sekta za biashara,” amesema.
Caroline amesema ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye kazi huleta tija na ufanisi bora kazini kutokana na weledi walionao, na namna wanavyojituma kazini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Jonas Lubago amesema jukwaa hilo ni mwarobaini wa tatizo la ajira kwa wenye ulemavu.
“Sisi tuna changamoto ya kuajiriwa, tumejaribu kuwapa mafunzo waajiri ili waweze kuajiri wenye ulemavu, tumebaini wana ubaguzi wanaona mazingira yao sio rafiki kuajiri wenye ulemavu, mtandao huu ni mwarobaini tutakwenda kuwaonyesha waajiri uwezo wa watu wenye ulemavu,” amesema.
Lunago amesema ni muhimu Serikali na sekta binafsi zinazowatetea wenye ulemavu kufuatilia utekelezaji wa sheria inayowataka waajiri kuwa na watu wenye ulemavu katika taasisi zao.
Sheria anayoikumbusha Lugano ni watu wenye ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 na kifungu cha 31 cha Sheria hiyo inayoelekeza kila mwajiri anayeajiri kuanzia watu 20, kuhakikisha asilimia 3 ya waajiriwa wake ni wenye ulemavu.
Amesema takwa hilo la kisheria la kuwa na wenye ulemavu kwenye ajira ni muhimu kila mwaka kufanyike tathimini kuangalia utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema Serikali inawathamini watu wenye ulemavu, na katika fursa za ajira zinapotangazwa kundi hilo haliachwi nyuma.
Amesema katika ajira ambazo Serikali imekuwa ikizitangaza hivi karibuni watu wenye ulemavu 1,500 wamepewa kipaumbele.
“Tunatoa msisitizo kwa sekta binafsi kuamini makundi ya watu wenye ulemavu,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Sightsavers International wanatekeleza mradi wa uwezeshaji kiuchumi kwa watu wenye ulemavu, lengo ni kuongeza ufikikaji wa ajira rasmi na ujumuishaji katika sehemu za kazi kwa kundi hilo.
“Mradi huo unalenga kuwajengea uwezo wanawake na wanaume wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika fursa za uwezeshaji kiuchumi, kuboresha uelewa na kuwajengea ujasiri waajiri walioko sekta binafsi ili watengeneze mazingira jumuishi mahali pa kazi kuendana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu (UNCRPD, kifungu cha 27,” amesema.
Kupitia mtandao uliozinduliwa, Suzanne amesema waajiri walioko katika sekta binafsi hukutana kushirikishana uzoefu, kujifunza na kufanya kazi ya pamoja ya kuendeleza ajenda ya ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu mahali pa kazi.