
Arusha. Wakati Serikali ikitekeleza sera mpya ya elimu iliyojikita katika elimu ya amali, wasichana walio kwenye rika balehe wametakiwa kunufaika nayo ili kuleta uwiano sawa katika ajira.
Sera hiyo mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023, imetoa kipaumbele katika elimu ya ufundi kama mwarobaini wa ajira kwa vijana.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Machi 7, 2025 na Mwakilishi wa Jumuiya ya Vyuo na Taasisi za Ufundi Canada (CICan) ambaye pia ni Mshauri Mkuu wa Mradi wa Uwezeshaji kupitia Ujuzi (ESP), Dk Alice Mumbi kwenye mkutano wake na vyombo vya habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo kitaifa yatafanyika kesho jijini Arusha.
Amesema kupitia mradi wa ESP kwa kushirikiana na Serikali, wameweza kupunguza vikwazo vinavyozuia ushiriki wa wanawake vijana katika mafunzo ya ujuzi.
Amesema lengo la mradi ni kuinua kizazi kipya hasa vijana wakiwemo wasichana balehe na wanawake vijana kama nguvu ya mabadiliko ya kudumu.
Dk Mumbi amesema mradi huo unaungana na juhudi za Serikali katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani yenye kaulimbiu isemayo: “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.”
Amesema kaulimbiu hii inalenga kuinua kizazi kipya hasa vijana wakiwemo wasichana balehe na wanawake vijana kama nguvu ya mabadiliko ya kudumu.
Amesema kupitia ushirikiano huo na Serikali, ESP imefanikiwa kuondoa vikwazo vikubwa vinavyozuia ushiriki wa wanawake vijana katika mafunzo ya ujuzi.
“Hii imefanyika kupitia maboresho ya vituo vya malezi ya watoto katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs), hatua hii imeongeza upatikanaji wa elimu bora kwa wanawake na wasichana wengi zaidi pamoja na wale walio katika mazingira magumu,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Ushiriki wetu unathibitisha dhamira yetu ya kuendeleza usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha wanawake na wasichana kupata ujuzi wanaohitaji ili kustawi kiuchumi.
“Kupitia ushirikiano na Serikali ya Tanzania na wadau wetu, tunakabiliana na vikwazo ambavyo kwa muda mrefu vimezuia wanawake wa Kitanzania kupata elimu, mafunzo na fursa za ajira.”
Dk Mumbi amesema wanawake na wasichana wanapowezeshwa kwa ujuzi, hawabadilishi tu maisha yao, bali pia wanachochea maendeleo endelevu katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Amefafanua kuwa mradi huo wa miaka saba ulioanza mwaka 2021 utafikia wanawake 20,000.
Awali, Mkufunzi wa ufundi magari na mratibu wa mradi wa ESP eneo la Mto wa Mbu wilayani Monduli, Mariam Msita amesema ni muhimu wasichana kuendelea kujengewa uwezo kwa lengo la kujiinua na kutumia fursa mbalimbali zilizopo.