Mwanzo mwisho kuachiwa huru kwa aliyehukumiwa maisha kwa kumbaka mkewe

Arusha. Mahakama ya Rufani imemuachia huru, Shauri Vungwa aliyekuwa amehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela na viboko 12, baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mke wake aliyekuwa na umri wa miaka 46.

Awali Mbele ya Mahakama ya wilaya ilidaiwa Juni 10,2017,katika Kijiji cha Mamba Wilaya ya Chunya na Mkoa wa Mbeya, mrufani alimbaka, kumlawiti na kisha kuingiza mko wake kwenye uke wa mkewe na kutoa nje mfuko wa uzazi.

Hukumu ya rufaa hiyo iliyomwachia huru Shauri ilitolewa Aprili 17,2025 na jopo la majaji watatu ambao ni Winfrida Korosso, Panterin Kente na Leila Mgonya walioketi Mbeya.

Rufaa hiyo iliungwa mkono na upande wa Jamhuri ambao waliieleza Mahakama kuwa ushahidi unaonesha kuwa, mrufani alitenda makosa zaidi ya moja ambayo ni ubakaji, kulawiti na kushambulia mara moja ila shitaka lililopo ni ubakaji pekee na kuiomba Mahakama iruhusu rufaa hiyo.

Majaji hao baada ya kupitia mwenendo na sababu za rufaa hiyo walibaini upande wa mashitaka haukuthibitisha vipengele muhimu vya shitaka dhidi ya mrufani, na kushikilia kuwa kosa la ubakaji halikuthibitishwa bila ya shaka yoyote dhidi ya mrufani na kumwachia huru.

Rufaa hiyo ya pili inatokana na rufaa ya kwanza ya mwaka 2019,ambapo Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, ilitupilia mbali rufaa ya kwanza aliyokuwa ameitaka Shauri.

Msingi wa rufaa

Awali Shauri alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Chunya kwa kosa la ubakaji kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(a) na 131(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela na viboko 12.

Mbele ya Mahakama ya wilaya ilidaiwa Juni 10,2017,katika Kijiji cha Mamba Wilaya ya Chunya na Mkoa wa Mbeya, mrufani alimbaka mkewe aliyekuwa na umri wa miaka 46.

Mwathirika wa tukio hilo ambaye alikuwa shahidi wa kwanza wa Jamhuri, alifiwa na mume wake mwaka 2008 na mwaka 2015 alikutana na Shauri ambaye alikuwa mkulima mwenzake, wakawa wapenzi kisha  wakaoana mwaka huohuo.

Aliieleza Mahakama kuwa kadri muda ulivyokuwa ukienda, uhusiano baina yao ulizidi kuwa mbaya kwani Shauri alikuwa akimpiga.

Alieleza siku ya tukio, Shauri alipomkuta nyumbani alianza kumtukana, akachana suruali aliyokuwa amevaa, akambaka, kumlawiti kisha akaingiza mkono kwenye uke wake na kutoa mfuko wa uzazi.

Alisema kuwa aliripoti tukio hilo kwa shahidi wa tatu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kitongoji, kisha kituo cha Polisi Lupa.

Shahidi wa pili, Dk Kitazi aliieleza Mahakama kuwa Juni 11,2017 alishuhudia mwathirika wa tukio hilo akiwa anatetemeka na kushindwa kuketi kutokana na maumivu makali aliyokuwa nayo.

Alieleza kuwa alichunguza sehemu za siri za shahidi huyo wa kwanza, akakuta uke wake ukiwa na uvimbe na damu na kuwa mfuko wa uzazi ulikuwa nje ya uke, na kutokana na hali hiyo alimpatia huduma ya kwanza kisha kumpeleka Hospitali ya wilaya kwa matibabu zaidi.

Shahidi wa tatu, alishuhudia kuwa mrufani na shahidi wa kwanza walikuwa wakiishi kama mke na mume, ila baadaye walikuwa na ugomvi uliohusisha kupigwa na kulazimika kutatua baadhi ya migogoro baina yao.

Alieleza Juni 10,2017,saa tano usiku, shahidi wa kwanza alienda nyumbani kwake huku akivuja damu kwenye sehemu zake za siri ambapo yeye na mkewe wakiwa bado wanashangaa nini kimetokea.

Alieleza shahidi wa kwanza aliwaonyesha uke wake ambapo waliona mfuko wa uzazi ukining’inia hali iliyowafanya wampe huduma ya kwanza na siku iliyofuata wakampeleka kituo cha Polisi.

Alieleza kuwa shahidi wa kwanza alipata fomu ya PF3 na kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Chunya, ambapo shahidi wa nne, Anjensi Mwansasu alimfanyia uchunguzi wa kiafya na kubaini mfuko wa kizazi ulikuwa nje ya sehemu zake za siri.

Kwa upande wake shahidi wa tano, Ofisa wa Polisi katika ushahidi wake mfupi alieleza Mahakama kuwa alimhoji mrufani Julai 6, 2017 na baada ya uchunguzi wa kina ushahidi kwenye rekodi ulithibitisha kosa la ubakaji.

Katika utetezi wake, Shauri alikana kutenda kosa hilo na kusema kuwa mkewe alitengeneza kesi dhidi yake ili atumie mapato yao ya kilimo peke yake.

Mahakama ya Wilaya ya Chunya, ilihitimisha kwamba, kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila shaka yoyote, alipatikana na hatia kama alivyoshtakiwa, kutiwa hatiani na kuhukumiwa kama ilivyoelezwa hapo juu.

Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ilitupilia mbali rufaa ya kwanza ya Shauri na kubariki adhabu aliyokuwa amepewa.

Katika rufaa ya pili, Mahakama ya Rufani, Shauri alikuwa na sababu nne za rufaa ambazo ni Mahakama ya kwanza ya Rufaa ilikosea kisheria ilipotupilia mbali rufaa ya mrufani huku upande wa mashitaka ukishindwa kuthibitisha shitaka hilo pasipo shaka.

Nyingine ni kulikuwa na baadhi ya tofauti kati ya mashahidi wa upande wa mashitaka katika kuthibitisha kesi.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo Shauri hakuwa na uwakilishi wa Wakili huku upande wa Jamhuri ukiwalikishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Caroline Matemu.

Wakili Matemu alieleza Mahakama kuwa anaunga mkono rufaa hiyo kwa kuwa shitaka hilo halikuthibitishwa bila shaka yoyote.

Aliielekeza Mahakama kwenye ukurasa wa nane aya ya tatu ya kumbukumbu ya rufaa na kudai kuwa mrufani alikuwa mume wa mwathirika wa tukio hilo, ila hakuna popote panapoonyesha walitenganishwa.

Wakili huyo alikwenda mbele zaidi kueleza kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 130 (2) (a) cha Kanuni ya Adhabu, mtu anaweza kutenda kosa la ubakaji kwa mwanamke ambaye si mke wake au ikiwa wametengana.

Alifafanua kuwa, ushahidi wa upande wa mashitaka unaonyesha kuwa, mrufani alitenda makosa zaidi ya moja ambayo ni ubakaji, kulawiti na kushambulia mara moja ila shitaka lililopo ni ubakaji pekee na kuiomba Mahakama iruhusu rufaa hiyo.

Shauri alipopewa nafasi ya kujieleza tena, hakuwa na lolote la kuongeza na kuomba Mahakama kuruhusu rufaa yake na kumwachia huru.

Uamuzi Majaji

Jaji Mgonya amesema upande wa Jamhuri uliunga rufaa hiyo mkono kwa sababu mrufani na mwathirika walikuwa mke na mume ambao hawakuwa wametengana.

Jaji amesema Shauri alishtakiwa na kutiwa hatiani kwa kosa la ubakaji kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(a) na 131 cha Kanuni ya Adhabu Kifungu cha 130(1)(2)(a) cha Kanuni ya Adhabu kinachohusisha mambo matatu.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni mwanaume kufanya tendo la ndoa na msichana au mwanamke, mwanamke huyo hapaswi kuwa mke wake au ikiwa ni lazima wawe wametengana wakati madai ya ubakaji yalipofanywa na tatu kwamba mwanamke hakukubali kujamiiana.

“Haya ni mambo muhimu ya kosa ambayo yalipaswa kuanzishwa na upande wa mashitaka, kutokana na hayo hapo juu ni dhahiri kwamba, nchini Tanzania suala la ubakaji katika ndoa na hitaji la mwanamke aliyeolewa kupata ridhaa ya kufanya mapenzi na mumewe halitambuliwi kabisa na sheria,” amesema Jaji

“Sheria inatambua ubakaji wa ndoa pale tu mume anapojamiiana na mke wake ambaye ametengana naye bila yeye kuridhia. Tazama Rufaa ya jinai namba 226 ya mwaka 2021 ya  July Joseph dhidi ya Jamhuri, iliyotolewa Juni 8,2022,”ameongeza

Jaji Mgonya amesema kutokana na msimamo huo wa kisheria wanalazimika kukubaliana na msimamo wa Wakili wa Serikali kwamba kosa la ubakaji halikuthibitishwa kwa kiwango kinachohitajika dhidi ya mrufani.

Amesema sababu ya msimamo wao ni katika kumbukumbu kwamba, mwathirika alikuwa mke wa mrufani ambaye yeye mwenyewe katika ushahidi wake ameeleza walifunga ndoa mwaka 2015,ushahidi ulioungwa mkono na shahidi wa tatu ambaye aliwahi kutatua migogoro yao ya ndoa.

“Ni jambo la kawaida kwamba, upande wa mashitaka unalazimika kuonyesha kwamba vipengele vyote vya kosa vimeanzishwa, pia lazima tusisitize tena kwamba, katika kesi za jinai upande wa mashitaka unalazimika kuthibitisha kesi bila shaka yoyote, “

Jaji Mgonya amesema kuhusu utofauti kati ya mashahidi wa upande wa mashitaka katika kuthibitisha kesi hiyo, wakipitia kumbukumbu za rufaa hiyo wanaona mkanganyiko upo kwani kumbukumbu zinaonyesha Juni 11,2017 mwathirika wa tukio hilo alipewa PF3 akatibiwa zahanati ya Mamba.

Jaji amesema shahidi wa pili aliieleza Mahakama kuwa mwathirika alikuwa na maumivu makali kwani mfuko wa uzazi ulikuwa umevimba na kutoka nje, alimpatia huduma ya kwanza na kumpeleka Hospitali ya wilaya kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo, ilibainika kuwa, mwathirika hakwenda huko mara moja kwa sababu hakuwa na pesa na siku iliyofuata alirudi zahanati na kumweleza shahidi wa pili kuwa hana maumivu tena.

Jaji amesema kutokana na kipande hicho cha ushahidi, wanakuta kuna utata kati ya mashahidi wa upande wa mashitaka hasa ushahidi wa shahidi wa pili na wa nne ambao wote walieleza kumhudumia mwathirika huyo.

“Malalamiko hayo hapo juu ya mrufani yanatosha kuondoa rufaa yote, bila kuangalia sababu zingine za rufaa, tunafuta hukumu na kuweka kando adhabu aliyopewa na kuruhusu rufaa hii, tunaagiza mrufani aachiliwe huru mara moja isipokuwa kama ameshikiliwa kwa sababu nyingine halali,” amehitimisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *