
Elias Mwanjala amerejea kukiongoza Chama Cha Soka Mbeya (MREFA) huku akizitaja Tanzania Prisons, KenGold na Mbeya City akisisitiza lazima mpira uchezwe upya.
Mwanjala aliwahi kuongoza chama hicho kwa miaka nane kuanzia 2012 hadi 2020 kabla ya kufungiwa kujihusisha na mpira wa miguu ambapo kifungo hicho kilimalizika 2023 na leo Aprili 6, 2025 amechaguliwa nafasi ya mwenyekiti kwa kura zote za ndiyo baada ya aliyekuwa mpinzani wake, Sadiki Jumbe aliyekuwa anatetea nafasi hiyo kuondoshwa wakati wa usaili kutokana na kukosa vigezo.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Mwanjala amesema anahitaji kuona mpira ukichezwa akieleza kwa sasa anasikitika kuona timu za mkoani humo zikichechemea kwa matokeo yasiyoridhisha kwenye Ligi Kuu Bara.
Ameagiza pia vyama vya soka Wilaya za Kyela, Mbarali, Mbeya Mjini na Mbeya Vijijini kurudia uchaguzi baada ya uchaguzi uliopita kuwa batili akifafanua kwa sasa viongozi waliokuwepo waendelee hadi uchaguzi utakapoisha.
“Naamini mpira wa Mbeya sasa utaenda kuchezwa, tuzipe nguvu timu zetu Prisons, KenGold na Mbeya City tuone zinafikia malengo, hapo nyuma mambo yamekuwa magumu sana lazima tubadilike,” amesema Mwanjala.
Amewaomba wadau mbalimbali kurejesha nguvu mpya kwenye soka la Mbeya kusaidia vijana kufikia ndoto zao katika michezo akiahidi mafanikio kwenye uongozi wake.
Kwa upande wa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu (TFF), Mohamed Mashango amejiondoa dakika za mwisho na mpinzani wake Geofrey Mkumbwa kupita kwa kura zote tisa.
Naye mjumbe wa kamati tendaji ya chama hicho, Elisia Mwaipopo amesema wanaenda kuanza upya wakishirikiana na mwenyekiti kuhakikisha soka la Mbeya linakuwa na mabadiliko.
“Tunaomba ushirikiano kwa wadau wote na matarajio yetu ni kuona tunafikia malengo, tutatoa ushirikiano kadri ya uwezo kuhakikisha soka letu linapiga hatua kwa ngazi zote,” amesema Elisia.
Mwanjala kabla ya kuondoka madarakani, aliacha timu nne zikishiriki Ligi Kuu Bara ambazo ni Tanzania Prisons, Mbeya City na Mbeya Kwanza (kwa sasa ipo Championship), na Ihefu iliyouzwa na sasa ikijulikana Singida Black Stars.
Kiongozi huyo amerejea akizikuta Tanzania Prisons na KenGold iliyopanda daraja msimu huu zikipambana kujinusuru na janga la kushuka daraja kwenye Ligi Kuu.