Dar es Salaam. Kwenye biashara, robo ya nne ya mwaka, ambayo kimsingi ni miezi minne ya mwisho wa mwaka ni wakati wa “kufunga mahesabu ya duka.”
Ni kipindi cha kutathmini mwenendo wa benki kwa mwaka mzima dhidi ya malengo yaliyowekwa na uongozi wa taasisi. Mwanga Hakika Bank ni miongoni mwa benki chache zilizofanya vizuri katika robo ya mwisho ya mwaka wa fedha 2023/24.
Katika taarifa yake ya kifedha iliyochapishwa hivi karibuni, benki hiyo imetia fora kwenye vipimo vya kiutendaji wa benki kwa mwaka husika kuanzia kwenye faida ya benki, jumla ya mali, amana za wateja, mikopo halisi, mapato ya riba na yasiyo ya riba.
Katika kipindi hicho, faida kabla ya kodi imefikia Sh 15 bilioni katika mwaka 2024 kutoka Sh 10 bilioni mwaka wa fedha 2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia 52.67. Mali za benki zimekua kufikia Sh Sh325 bilioni kwa mwaka 2024 kutoka Sh 208 bilioni kwa mwaka 2023, ongezeko la asilimia 56.60.
Jalada la mikopo limefikia thamani ya Sh 200 bilioni kwa mwaka 2024 kutoka Sh 131 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023, sawa na ongezeko la asilimia 52.19 Amana za wateja zimepanda na kufikia Sh 217 bilioni kwa mwaka 2024 kutoka Sh 142 bilioni kwa mwaka 2023, sawa na ongezeko la asimilia 53.24.
Pia, mapato yasiyo ya riba yamekua kufikia kufikia Sh 10 bilioni kwa mwaka 2024 kutoka Sh 7.2 bilioni kwa mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 37.3.
Wakati viashiria hivyo muhimu vya benki vikukua, mikopo chechefu ya benki imeshuka hadi asilimia 0.87 kwa mwaka 2024 kutoka asilimia 1.74 kwa mwaka 2023, sawa na anguko la asilimia 50.20.
Akizungumza ofisini kwake, Makumbusho, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa Mwanga Hakika Bank, Chomete Hussein anasema kuwa mwenendo huo wa benki unaashiria kukubalika kwao kwa wateja.
“Ukuaji wa amana wa asilimia 53, kutoka Sh 142 bilioni hadi Sh 200 bilioni ni kiashiria cha kwamba wateja wanaamini katika bidhaa na huduma zetu,” anaeleza Hussein.
Ukuaji wa jumla ya mali za benki wa asilimia 56.60, unatuma ujumbe kuwa benki hiyo ndiyo inayokua kwa kasi kwa sasa nchini kwa miaka miwili mfululizo, anasisitiza.
“Utekelezaji mikakati ya benki iliyopo chini ya bodi ya wakurugenzi sambamba na ubora wa bidhaa umekuwa na nafasi kubwa katika matokeo haya,” anaeleza zaidi Hussein.
Pamoja na sababu za ndani za utendaji wa benki, anaamini pia mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara yaliyowekwa na Serikali yamechangia wao kufikia hapo.
Kama hiyo haitoshi, anasema usimamizi mzuri katika sekta ya fedha unaofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni siri nyingine iliyo nyuma ya hatua hiyo kubwa iliyopigwa na Mwanga Hakika Bank.

Sehemu maalumu ya wateja na wageni kusubiria huduma katika Benki ya Mwanga Hakika.
Akizungumzia matokeo mazuri ya benki hayo katika mikopo chechefu, anasema kuwa kama benki wamewezesha wafanyabiashara kukopa kiasi cha fedha kinachoweza kuwasaidia kukuza biashara zao ili baadaye warejeshe kwa wakati.
“Ikitokea mkopaji anakopa halafu anakutana viashiria vingine vya hatari kama vile mdororo wa kiuchumi au majanga au anapoachishwa kazi, inakuwa ngumu kulipa mkopo na kusababisha mkopo chechefu,” anaongeza.
Uimarikaji wa uchumi, usalama wa ajira za wakopaji na uwezo wa watu kutimiza malengo yao, kumesaidia kushuka kwa viwango vya mikopo hiyo chini zaidi ya ukomo uliowekwa kisheria na BoT wa kutokuzidi asilimia tano, hizi zikiwa sababu za nje.
Ukiingia ndani, anasema ni usimamizi mzuri wa mikopo wa benki kuanzia kwenye kutambua biashara za wateja, mahitaji, kiasi cha mkopo na ufuatiliaji wa matumizi ya mkopo na urejeshaji.
“Ukopeshaji kiasi kidogo au ukopeshaji kiasi kikubwa zaidi ni sababu ya kuwa na mikopo chechefu; haya ni mambo ambayo kama benki tunayaepuka,” anaeleza Ofisa huyo.
Kutokana na rekodi inazoshikilia za kuwa benki inayokua kwa kasi zaidi, anasema hiyo inawapa fursa ya kuendelea kuleta bidhaa bora zinazokidhi mahitaji halisi ya Watanzania.
Fursa zilizotazamwa sokoni
Mwanga Hakika Bank imeona fursa katika maeneo matatu ya kibiashara; uwekezaji katika teknolojia za kisasa, kundi la wafanyabiashara wadogo na kati na wakandarasi, kulingana na Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa benki hiyo.
“Kuna uwekezaji mkubwa wa kidijitali ambao benki inaufanya, ikitoka kwenye majengo kwenda digital, kuhakikisha tunawafikiwa wateja wengi kwa njia ya kidijitali.
“Kundi la SMEs ni kubwa sana hatuwezi kulimaliza lakini ndiyo linaloendesha uchumi wowote ule duniani. Tunatengeneza bidhaa zinazokidhi mahitaji yao kuhudumia soko hili. Ni soko ambalo limetusaidia kukua kwa kasi zaidi.
Wakandarasi ni eneo lingine tunaloliangalia kwa makini. Hawa ni wateja wetu kwa muda mrefu na tutaendelea kuwapa kilicho bora,” anadadavua.
Ujumuishi wa kifedha
Anasema mpango wa benki ni kutanua shughuli zake ndani na nje ya mipaka ya nchi licha ya ukweli kwamba upanuzi wake unaangaliwa katika mfumo wa kidijitali, kwa kuangalia mwelekeo wa dunia nzima katika sekta ya fedha.
Anakiri kuwa upanuzi wa matawi hautaachwa na bado ni sehemu ya mkakati wake ambapo baada ya kuisha kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025, wataeleza wapi wanakwenda kufungua matawi. Hivi sasa benki hiyo ina jumla ya matawi saba pekee nchi nzima.
“Mafundi wako chini huko wanaendelea na ujenzi, tukikutana quarter (robo) ya kwanza, mtajua tunakwenda wapi na wapi,” anaeleza zaidi.
Mwelekeo wa benki
Mkakati uliopo ni kufanya maboresho makubwa ya bidhaa za benki ambazo kimsingi huwa hazibadiliki duniani kote. Anasema maboresho yatakayofanyika yanahusu Mobile App itakayokuwa na uwezo wa kumpa mteja uzoefu mpya na wa aina yake.
Kingine kinachofanyika, anasema, ni kuendelea kubuni na kuongeza ufanisi wa bidhaa na huduma wanazozitoa kwa wateja.
Changamoto
Hussein anasema kuwa mwaka 2024, soko la huduma za benki lilikabiliwa na changamoto ya ukwasi, kusababisha kupanda kwa gharama za utunzaji amana za wateja na kuathiri kiwango cha faida ya benki.
Na moja ya ufumbuzi wake, anasema ni kuendelea kuhimiza watu kuweka fedha zao katika mfumo wa kibenki na kuachana na kuhifadhi majumbani.
“Kukusanya amana kila benki inafanya hivyo, lakini unamrahisishiaje mtu kukupa amana. Tulifanya ubunifu mkubwa katika kukusanya amana kupitia mifumo mipya ya malipo. Kwa kufanya hivyo, ukwasi katika benki uliongezeka.”
Shida nyingine ni uhaba wa Dola. Kwa robo tatu yote ya mwaka 2024, Dola ya Marekani iliadimika na kuathiri kiasi kikubwa soko la fedha duniani kote.
Serikali ilipambana kuleta utulivu wa Shilingi kutokana na kukosekana kwa Dola, na wadau kama Mwanga Hakika Bank, walisaidia kuondoa utegemezi wa Dola kwenye uchumi kwa kuleta bidhaa mahsusi kwa wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi kupitia fedha za mikopo ya biashara.
Anasema Watanzania watarajie bidhaa bora za kibenki zinazotatua changamoto zao kama ilivyo kawaida yao. Pia, ufanisi na ubunifu utaongezeka maradufu ili kuendelea kuwahudumia wateja wao.
Kwa wafanyakazi wao, matokeo haya mazuri ni kielelezo cha jasho na nguvu waliyoiweka katika kuhakikisha benki yao inafanya vyema. Mchango wao unathaminiwa.