
Nairobi. Mahakama ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JKIA chini ya Hakimu Mkuu Irene Gichobi, imemuachia kwa dhamana mwanasiasa wa Kenya, Philip Aroko anayetuhumiwa katika mauaji ya Mbunge, Charles Were.
Mbunge Were aliuawa Aprili 30, 2025 kwa kupigwa risasi na watu waliokuwa kwenye pikipiki katika barabara ya Ngong jijini Nairobi.
Kwa mujibu wa tovuti ya KBC, gari ya mbunge huyo aina ya Toyota Crown ilisimama baada ya taa za barabarani nyekundu kuwaka kabla ya watu hao kusogelea gari kisha kutoa bastola na kumfyatulia risasi.
Kufuatia mauaji hayo mwanasiasa huyo alikamatwa na kuzuiliwa kwa siku saba na katika uamuzi wake, Hakimu Gichobi amemzuia Aroko kusafiri kuelekea Kaunti ya Homa Bay, ambayo ni nyumbani kwa marehemu mbunge huyo.
Hivyo Mahakama imemuachia Aroko kwa dhamana ya pesa taslimu ya KSh 300,000 sawa na Sh6,259,198 za Kitanzania huku Hakimu Gichobi alikataa ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), lililotaka Aroko azuiliwe kwa siku saba zaidi. Kwa mujibu wa Tuko ya nchini humo.
Katika uamuzi wake, alielekeza masharti kadhaa kwa Aroko, ikiwa ni pamoja na kutakiwa kukabidhi pasipoti yake mahakamani na kupigwa marufuku kusafiri kwenda Kaunti ya Homa Bay, ambako ndipo nyumbani kwa marehemu Were.
Aidha, Mahakama imempiga marufuku kuwasiliana na familia ya marehemu, washukiwa wengine au mtu yeyote anayehusiana na kesi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti ya Citizen TV, Mahakama pia imeamuru asiingilie au kuharibu ushahidi wowote unaohusiana na uchunguzi unaoendelea.
Kama sehemu ya masharti ya dhamana, mwanasiasa huyo kutoka Kasipul ameagizwa kuripoti mara kwa mara kwa maofisa wa uchunguzi na kutoa ushahidi wowote utakaohitajika kuhusiana na kesi hiyo.
Vilevile katika hatua nyingine kuhusu mwanasiasa huyo, ambaye ana nia ya kuwania ubunge wa Kasipul, washukiwa watano wanaohusishwa na mauaji walifikishwa mbele ya hakimu katika Mahakama ya JKIA. Upande wa mashitaka umesema wanaendelea kuchunguza miamala ya kifedha inayodaiwa kuhusishwa na Aroko, ambayo inashukiwa kufadhili uhalifu huo.
Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, alitangaza kuwa washukiwa 10 tayari wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya Were. Wakili Danstan Omari alidai kuwa mteja wake, Philip Aroko, alikamatwa ili kumzuia kuhudhuria mazishi ya Mbunge wa Kasipul.
Pia, Polisi ilisema imefanikiwa kupata bastola inayoshukiwa kutumika kwenye mauaji ya mbunge huyo baada ya msako mkali uliofanyika eneo la Chokaa huko Nairobi.