Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imesema mwanaharakati Greta Thunberg amefukuzwa kutoka nchini Israel siku ya Jumanne, siku moja baada ya Jeshi la wanamaji la Israel kulizuia kundi la wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina kuingia katika Ukanda wa Gaza.
Thunberg alikuwa mmoja wa abiria 12 kwenye mashua kwa jina Madleen, iliyokuwa imebeba misaada inayokusudiwa kwa watu wa Gaza inayokumbwa na vita.
Wanaharakati hao wamesema hatua yao ni ya kupinga vita vinavyoendelea Gaza na pia wanataka kuumulika zaidi mgogoro wa kibinadamu lakini Israel imesema meli kama hizo zinakiuka marufuku ya kuingia kwenye Bahari ya Ukanda wa Gaza.
Muungano wa Freedom Flotilla, ambao uliandaa safari hiyo, umesema wanaharakati hao walitekwa nyara na vikosi vya Israel walipokuwa wakijaribu kuwasilisha misaada inayohitajika sana katika Ukanda wa Gaza.
Soma pia: Wanajeshi wa Israel waizuia boti ya wanaharakati kufika Ukanda wa Gaza
Adala, kikundi cha wanasheria nchini Israel kinachomwakilisha Thunberg na wanaharakati wengine, kimethibitisha kwamba Thunberg raia wa Sweden, wanaharakati wengine wawili na mwandishi wa Habari walikubali hatua za kuwafukuza na kuondoka kutoka Israel lakini wanaharakati wengine walikataa na hivyo wamewekwa kizuizini na kesi yao imepangwa kusikilizwa na mamlaka za Israel.
Taarifa nyingine zinasema, Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, amesema, Hamas “lazima ikabidhi silaha zake” na ametoa wito wa kupelekwa vikosi vya kimataifa kuwalinda “watu wa Palestina”.
Katika barua aliyomwandikia Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ambao mwezi huu kwa Pamoja watakuwa wenyekiti wenza wa mkutano kuhusu suluhu ya mataifa mawili ya Israel na Palestina, Abbas ameeleza hatua kuu ambazo anadhani ni lazima zichukuliwe ili kukomesha vita huko Gaza na kufikia amani katika Mashariki ya Kati.
Wakati huo huo Tume huru ya Umoja wa Mataifa imesema leo Jumanne kwamba mashambulizi ya Israel yanayolenga shule, maeneo ya kidini na kitamaduni huko Gaza ni sawa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu unaokusudia kuwaangamiza Wapalestina.
Na vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na waasi wa Kihouthi nchini Yemen vimeripoti juu ya mashambulio ya Israel kwenye bandari ya Hodeida huku jeshi la Israel likisema kikosi chake cha wanamaji kimeshambulia eneo hilo baada ya kuwapa raia agizo la kuondoka kutoka kwenye bandari tatu zinazoshikiliwa na Wahouthi.
Israel imesema mashambulizi hayo ni kwa ajili ya kusitisha matumizi ya bandari hiyo kwa madhumuni ya kijeshi. Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema hilo ni onyo kwa magaidi wa Houthi kwamba ikiwa wataendelea na mashambulizi yao basi watakabiliwa kwa nguvu zote na watawekewa vizuizi vya majini na angani.
Soma pia: Netanyahu: Tutalipa kisasi dhidi ya Wahouthi
Wakati huo huo jeshi la Israel leo Jumanne limetoa amri kwa wakaazi wa vitongoji kadhaa kaskazini mwa Gaza, kuondoka kutoka kwenye maeneo hayo baada ya kulizuia kombora lililorushwa kutoka upande wa ardhi ya WaPalestina.
Vyanzo: AFP/AP