
Kampala. Mwanahabari mkongwe wa Uganda, Shaka Ssali amefariki dunia Machi 27, 2025, akiwa na miaka 71.
Ssali aliyefariki huko Virginia, Marekani, alipata umaarufu katika kipindi cha “Straight Talk Africa” katika Voice of America (VOA), ambacho alikiendesha kwa zaidi ya miongo miwili.
Katika kipindi chake cha utangazaji, Ssali alifanya mahojiano na viongozi mbalimbali wa Afrika, wachambuzi na wananchi wa kawaida, akiongoza mijadala kuhusu demokrasia, utawala bora na maendeleo barani Afrika.
Aidha, mwanabari huyo alivuma zaidi na kauli yake maarufu, “I’m profoundly honored and exceedingly humbled,” (Ninajivunia sana na kunyenyekea kwa kiwango kikubwa) iliyotambulika na wengi kama alama ya kipindi chake.
Septemba 2024, Ssali alitunukiwa Tuzo ya Mafanikio ya Maisha na Jumuiya ya Waganda wa Amerika Kaskazini (UNAA), ikitambua mchango wake katika tasnia ya habari barani Afrika.
Baada ya kustaafu kutoka VOA Mei 2021, aliendelea kushiriki katika shughuli za kuhamasisha na kutoa mwongozo kwa waandishi wa habari chipukizi.
Mwandishi wa Habari wa VOA, Harun Maruf kwenye ukurasa wa akaunti yake ya X (zamani Twitter) inasomeka: “Tunasikitika sana kutangaza kifo cha Shaka Ssali, mtangazaji wa muda mrefu wa Straight Talk Africa katika VOA. Ssali, mwandishi wa habari na mtangazaji mashuhuri, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 71, wiki mbili kabla ya kutimiza miaka 72, akiacha urithi usiofutika katika uandishi wa habari barani Afrika.”
“Kwa zaidi ya miongo miwili, Ssali alikuwa uso na sauti ya Straight Talk Africa, ambako aliwahoji viongozi wa Afrika, wachambuzi na raia katika mijadala muhimu kuhusu demokrasia, utawala, na maendeleo,”aliandika na kuongeza kuwa, “Mahojiano yake makini na kujitolea kwake kwa uhuru wa vyombo vya habari kulimpatia heshima kubwa kote barani Afrika na duniani. Mzaliwa wa Kabale, Uganda, maisha ya Ssali yaligubikwa na shauku ya kutafuta ukweli, uwajibikaji, na kuwawezesha vijana wa Afrika.
“Tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia yake, marafiki zake, na maelfu ya watazamaji waliomsikiliza kila wiki. Mchango wake katika uandishi wa habari na mijadala ya Afrika utaendelea kuishi kwa vizazi vijavyo. Kama alivyosema mara kwa mara ndugu Shaka Ssali, “Tuweke tumaini la Afrika hai.”
Kifo cha Ssali kimeshtua wana tasnia na wasio wana tasnia ya habari barani Afrika, huku salamu za rambirambi zikimiminika kutoka kwa marafiki na watu mbalimbali waliomfahamu.
Kwa zaidi ya miongo miwili, Shaka Ssali alikuwa maarufu katika vyombo vya habari barani Afrika, akifahamika kwa uandishi wake wa habari usio na woga.
Kupitia Straight Talk Africa, alizungumzia masuala mbalimbali yanayoikabili Afrika, kuanzia siasa, ufisadi hadi haki za kijamii na haki za binadamu. Mtindo wake wa kipekee, uliounganisha ucheshi, hekima na udadisi, ulimfanya kuwa kipenzi cha wasikilizaji.
Ssali ni nani?
Maarufu kama ‘Kabale Kid’, Ssali alizaliwa katika Wilaya ya Kabale nchini Uganda.
Katika safari ya maisha yake, Ssali aliwahi kuhudumu jeshini, kabla ya kuhamia Marekani, ambako alisoma na kupata Shahada ya Uzamivu (PhD) kwenye Mawasiliano ya Utamaduni mbalimbali kutoka Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA).
Mei 2021, Ssali alistaafu VOA, baada ya kufanya kazi kwa miaka 29, ikiwa ni pamoja na zaidi ya miongo miwili kama mwanzilishi, mtangazaji na mhariri mkuu wa kipindi cha ‘Straight Talk Africa’.
Kipindi hicho kilitoa jukwaa muhimu kwa viongozi wa Afrika, wachambuzi, na wananchi kujadili masuala ya demokrasia, utawala, na maendeleo ya bara hilo.
Katika taaluma yake, Ssali alifanya mahojiano na viongozi wakuu wa Afrika, wakiwemo marais na mawaziri wakuu wa nchi mbalimbali, huku akihakikisha sauti za wananchi wa kawaida zinajumuishwa katika mijadala kuhusu uongozi na maendeleo.
Aprili 2024, zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kifo chake, lakini alizikanusha kwa video, akitania kwa kusema, “Taarifa kuhusu kifo changu zimepotoshwa kwa kiwango kikubwa.”
Shaka Ssali atakumbukwa kwa maisha yake yenye mafanikio makubwa, Shaka Ssali alipokea tuzo na heshima nyingi kwa mchango wake katika taaluma ya uandishi wa habari.
Alikuwa gwiji wa taaluma ya uandishi wa habari na urithi wake utaendelea kuwahamasisha waandishi wa habari na watangazaji wa kizazi kijacho.