Dar es Salaam. Mwanafunzi wa Chuo cha Koteti kilichopo mkoani Tanga, Bonus Mbono (21) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa TikTok na kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine.
Mshtakiwa amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu, Machi 10, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 5907 ya mwaka 2025.
Amesomewa mashtaka hayo, wakili wa Serikali Erick Kamala, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga.
Kabla ya kusomewa mashtaka yake, Hakimu Mwankuga alimueleza mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi labda kwa kibali maalumu.

Mwanafunzi wa Chuo cha Koteti kilichopo mkoani Tanga, Bonus Mbono (21) akiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu Machi 10, 2025. Picha na Hadija Jumanne
Baada ya kueleza hayo, aliruhusu upande wa mashtaka kumsomea mashtaka yake mshtakiwa huyo.
Katika shtaka la kwanza, Kamala amedai Februari 8, 2025 sehemu isiyofahamika, mshtakiwa alichapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok, kwa kuhariri video ya Mwalimu Julius Nyerere akitoa kichwa nje na kurudisha ndani katika noti ya Sh1000, wakati akijua kuwa ni uongo.
Shtaka la pili, tarehe na siku hiyo katika eneo lisilofahamika, mshtakiwa alitumia kifaa haramu cha Pix Vase kutengeneza chapisho lenye taarifa za uongo na kurusha kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok, wakati akijua kuwa ni kosa kisheria.
Shtaka la tatu, Mbono anadaiwa Februari 10, 2025, katika Chuo cha Koteti kilichopo mkoani Tanga, alitumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la Prisca Anthony, kinyume cha sheria na bila kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka, ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu Mwankuga ameahirisha kesi hiyo hadi April 10, 2025 kwa kutajwa na mshtakiwa na mshtakiwa yupo rumande.