…Mwambusi atibuliwa Arachuga

KIPIGO cha mabao 3-0 ilichopewa Coastal Union kutoka kwa Simba kimemtibulia kocha wa timu hiyo, Juma Mwambusi rekodi aliyokuwa nayo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Mara ya mwisho Coastal kupoteza katika uwanja huo ilikuwa dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga Oktoba 26 mwaka jana walipolala bao 1-0, lakini baada ya hapo timu hiyo ilicheza mechi tano mfululizo na kushinda tatu, huku mbili zikiisha kwa sare.

Mechi hizo tano ambazo Coastal ilicheza mfululizo bila kupoteza ni pamoja na ile ya dhidi ya Kagera Sugar iliyowanyoa bao 1-0, Tanzania Prisons (2-1) na JKT Tanzania (2-1), kisha kutoka sare ya 1-1 dhidi ya KMC na suluhu ilipoumana na Azam, kabla ya Steven Mukwala juzi kumtibulia alipofunga hat trick wakati Simba ikishinda 3-0 na kuvunja rekodi hiyo ya kutofungwa mechi tano mfululizo.

Kipigo hicho bado kimeibakisha Coastal nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 24 baada ya mechi 22, ikishinda tano, ikipata sare tisa na kupoteza nane, ikifunga mabao 18 na kufungwa 23.

Akizungumzia kipigo hicho, kocha Mwambusi alisema bado anaamini timu yake ina nafasi ya kufanya vizuri katika mechi nane zilizosalia kufanya vizuri na kumaliza kwenye nafasi ambayo timu imewekea malengo.

“Hauwezi kushinda kila mchezo wapinzani wetu walitumia madhaifu ambayo yalijitokeza kwa upande wetu wakaweza kutuadhibu,” alisema Mwambusi.

Licha ya kuonekana kutofurahishwa na kipigo hicho kikubwa nyumbani ambayo imevunja tambo za muda mrefu za kutopoteza kwa maana ya kutoruhusu mpinzani kuondoka na pointi tatu Sheikh Amri Abeid kwa mechi tano mfululizo ila aliweka wazi atajipanga kwa mechi zingine.

Mwambusi ana kazi kubwa ya kuhakikisha Coastal inamaliza nafasi za juu katika Ligi ikiwemo nafasi ya nne ili kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa lakini wakati huo huo pia ana kazi ya kuinusuru timu hiyo isishuke daraja, kwani pointi ilizonazo haziiweki timu hiyo salama.

Coastal 6 zilizopita

Coastal 0-3 Simba

Namungo 0-0 Coastal

Coastal 0-0 Azam

Pamba Jiji 2-0 Coastal

Mashujaa 0-0 Coastal

Coastal 2-1 JKT TZ

Mechi zijazo Coastal

v Dodoma Jiji (ugenini)

v Kagera Sugar (ugenini)

v Yanga (ugenini)

v Singida BS (nyumbani)

v KenGold (nyumbani)

v TZ Prisons (ugenini)

v Fountain Gate (nyumbani)

v Tabora United (nyumbani)