
KOCHA wa Costal Union ya Tanga, Juma Mwambusi, ameshtukia kitu ndani ya timu hiyo huku akijipanga kukomaa na safu yake ya ulinzi iliyoonyesha dosari kubwa huku zikisalia mechi saba kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Hatua hiyo ya Mwambusi inakuja baada ya kikosi chake kujipima nguvu dhidi ya Taifa Stars, kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa hivi karibuni kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kupoteza kwa mabao 2-1.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwambusi alisema kupitia mchezo huo amegundua ana kazi ya kufanya kuhakikisha wanasuka safu imara ya ulinzi itakayoweza kuibeba timu yake pale wanapotangulia kupata bao.
Mwambusi ambaye ni kocha wa zamani wa Mbeya City, Yanga na Ihefu, alisema anataka kutumia siku zilizosalia tangu kusimama kwa ligi kuimarisha safu hiyo ya ulinzi kabla ya kuendelea kwa mechi za ligi.
“Safu ya ulinzi imeonyesha kuwa na changamoto katika kuzuia mabao, hili ni tatizo kubwa katika michezo za ligi na inatupa matokeo magumu na kukaa katika nafasi isiyoridhisha.
“Huu muda ambao umesalia tutaendelea kuyafanyia kazi haya kwa haraka ili kabla ya ratiba ya ligi kuendelea tuwe tumeimarika sawasawa kuhakikisha tunatoka kwenye eneo baya,” alisema Mwambusi.
Aidha, Mwambusi aliongeza kuwa, haridhishwi na nafasi ambayo Coastal Union inashikilia kwenye msimamo wa ligi, akisema inahitajika nguvu kubwa kuondoka hapo wakijipanga kuzitumia vizuri mechi zilizosalia.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu, Coastal Union inashikilia nafasi ya tisa ikikusanya pointi 25 baada ya kucheza mechi 23, ikifunga mabao 18 na kufungwa 23.