Marekani. Mkongwe wa Country Music, Dolly Parton (79) ameondokewa na mumewe, Carl Dean, 82, ambaye kwa miaka 59 waliishi pamoja ndani ya ndoa ambayo ilikuwa na mengi ya kujifunza lakini ikiacha maswali kwa baadhi ya watu!.
Alfariji ya Machi 3 kwa saa za Afrika Mashariki, mkali huyo wa kibao, Jolene (1973), kupitia ukurasa wake wa Instagram alitangaza kifo cha Dean kilichotokea huko Nashville, Marekani na kusema mazishi yake yataendeshwa kwa faragha.

“Dean na mimi tumetumia miaka mingi yenye msisimko pamoja. Maneno hayatoshi kuelezea upendo tuliokuwa nao kwa miaka zaidi ya 60. Asante kwa maombi yako na huruma,” sehemu ya ujumbe wa Dolly Parton ilieleza.
Kwa miaka mingi ya ndoa yao, hawakuwa watu wa kuongozana hata katika zile hafla kubwa na muhimu za Parton kama mwanamuziki mashuhuri duniani, na hata picha zao nyingi zinazopatikana mitandao ni zile walizopiga miaka ya 1980.
“Yeye hana wivu, na mimi pia sina wivu. Dean ndiye mwanaume pekee katika maisha yangu. Ningependa kuzeeka naye. Ikiwa atakufa kwanza, siwezi kuolewa tena. Upendo wangu kwake ni wa kina sana,” Parton aliiambia People mwaka 1981.
Wawili hao walikutana mwaka 1964 wakati huo Parton akiwa binti wa miaka 18 ambaye alikuwa akiishi na shangazi yake akimsaidia kulea mtoto. Dean alimuona Parton kwa mara ya kwanza pindi alipopeleka nguo kwa dobi na kuvutiwa naye kisha wakazungumza.
Kufikia Mei 30, 1966 wakafunga ndoa iliyohudhuriwa na watu wachache kama walivyotaka, upande wa Parton ni mama yake tu, Avie Lee Owens aliyefika katika kanisa la Ringgold Baptist huko Ringgold, Georgia ambapo shughuli hiyo ilifanyika.

“Nilisema, ‘lazima niwe na mama huko’, kwa hiyo nilikuwa nimenunua nguo chache, mama alikuwa ameninunulia Biblia yenye maua kadhaa juu yake, basi tukafunga ndoa siku ya Jumatatu,” alisema Parton, mtoto wa nne kati ya watoto 12 wa familia yao.
“Siku iliyofuata tulimsindikiza mama hadi kwenye kituo cha mabasi huko Chattanooga ili aweze kurudi Knoxville, kwa hiyo hakuwepo kwenye fungate yetu na ilitubidi sote turudi kazini asubuhi iliyofuata,” Parton aliiambia New York Times.
Kinachoshangaza baadhi ya watu katika ndoa hii, ni kwamba wanadai walipanga kutopata mtoto na hadi Dean anafariki ilikuwa hivyo, wakati wakitiza miaka 57 ya ndoa yao, Parton alidai hana majuto yoyote ya kuamua kutokuwa na mtoto maisha mwake!.
“Sijakosea kama nilivyofikiria, unajua mnapokuwa wanandoa wachanga, unafikiri mtapata watoto ila haikuwa moja wapo ya mambo yaliyonivutia sana. Nilikuwa na kazi yangu na muziki wangu na hivyo nilikuwa nikisafiri sana,” alisema na kuongeza.
“Nafurahi kuwa sikupata watoto, mimi na mume wangu, tunajifikiria tu kama watoto wa kila mmoja wetu, yeye ni mtoto wangu wa pekee, na mimi ni mtoto wake wa pekee. Siku zote nasema Mungu hakuniacha nipate watoto ili watoto wote wawe wangu,” alisema.
Hata hivyo, kwa miaka 30 sasa Parton amekuwa akiwasaidia mamilioni ya watoto duniani kupitia programu yake ya ‘Imagination Library’ ambayo inalenga kutoa misaada ya vitabu kwa watoto ambapo hadi sasa vitabu zaidi ya milioni 200 vimetolewa.
Dolly Parton aliyevuma kimuziki na albamu yake ya kwanza, Hello, I’m Dolly (1967), na hadi sasa akiwa ameuza rekodi zaidi milioni 100 duniani kote na kushinda tuzo 11 za Grammy, Forbes anakadiria utajiri wake kufikia Dola450 milioni.
Wimbo wake maarufu, Jolene (1973), ambao anamsisitiza mwanamke aliyemtaja kama Jolene kutomchukua mumewe, kisa cha wimbo huo kilitokana na dada mmoja ambaye alikuwa mhudumu wa benki ambaye alipenda kumchangamkia sana Dean.
Mwaka 2008 Parton aliiambia NPR kuwa mwanamke huyo alimfanya Dean kwenda benki kila wakati, ingawa hakuna kilichokuwa kinaendelea kati yao ila alitoa tu wimbo huo na jina la Jolene lilitoka kwa shabiki yake mmoja.

Utakumbuka Beyonce Knowles ameurudia wimbo huo (Jolene) na kuuweka katika albamu yake ya nane, Cowboy Carter (2024) ambayo ilikuja kushinda tuzo ya Grammy 2025 ikiwa ni mara ya kwanza kwake kushinda kipengele cha Albamu Bora.
Dean katika mahojiano na Entertainment Tonight mwaka 2016, alisema alipomuona Parton kwa mara ya kwanza hapo 1964, wazo lake la kwanza lilikuwa ni kwamba atamuoa msichana huyo maana ana sura nzuri na hiyo ndio siku ambayo maisha yake yalianza.
“Sikuwa na nia ya kuoa. Sikuwa na nia ya kupata mtu yeyote kwa wakati huo, lakini unajua jinsi upendo unavyoenda. Nashukuru Parton alielewa kwamba nilipaswa kufanya kile nilichokuja kufanya hapo baadaye,” alisema Dean.
Hata hivyo, uhusiano wao ulikuwa chanzo cha Parton kugombana na aliyekuwa meneja wake kipindi hicho, Fred Foster. Mwaka 2012, Parton alisema meneja wake hakutaka aolewe bali asimame na muziki wake kwanza kitu ambacho hakukubaliana naye.
Ikumbukwe Dolly Partorn ndiye aliyeandika wimbo ‘I Will Always Love You’ na kuurekodi mwaka 1973, baadaye 1992, Whitney Houston alikuja kuurudia ambapo ulitumia kama soundtrack ya filamu yake, The Bodyguard.
Toleo hili la Whitney aliyefariki mwaka 2012 ndilo maarufu zaidi, ulifanya vizuri ukushika namba moja chati za Billboard Hot 100 kwa wiki 14, ukishinda tuzo mbili za Grammy 1994 na hadi sasa unatambulika kama wimbo uliouza zaidi duniani kwa muda wote.