Mwalyanzi: Moto wa Mbeya City hauzimiki

KIUNGO mshambuliaji wa Mbeya City, Peter Mwalyanzi amesema ubora waliouonyesha katika Ligi ya Championship hautazimika kwani wamepania kuendelea nao hata kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na uwekezaji na umoja uliopo ndani ya timu hiyo.

Mbeya City imerejea Ligi Kuu Bara baada ya kukosekana kwa misimu miwili tangu iliposhuka 2022-2023, ikishika nafasi ya pili nyuma ya Mtibwa Sugar iliyobeba pia ubingwa wa Ligi ya Championship.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwalyanzi alisema uwekezaji mkubwa na umoja uliopo baina ya viongozi, wachezaji na benchi la ufundi ndio siri ya mafanikio ambayo pia yamechangia kuwarudisha mashabiki wa timu hiyo.

“Hatujaishia Championship moto utaendelea ule ule hadi Ligi Kuu msimu ujao Mbeya City imerudi upya tunakuja kukiwasha na kurudisha ushindani kama ilivyokuwa msimu wetu wa kwanza kucheza ligi,” alisema Mwalyanzi na kuongeza;

“Ubora wa timu unachangiwa na maelewano mazuri baina ya wachezaji, benchi la ufundi na viongozi ndio kitu kilichopo City kwa sasa na kila mmoja anahitaji mafanikio makubwa hivyo tumejenga timu na mshikamano.”

Mwalyanzi alisema wana Mbeya wameungana kuiweka kwenye ushindani timu yao na wanataka waione ikiwa bora na ndicho kilichofanyika kuanzia Championship.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *