Mwalimu mkuu mbaroni tuhuma za kumjeruhi mwanafunzi kwa kipigo

Shinyanga. Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia Erick Ombeni, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngilimba, kata ya Ulowa, wilayani Kahama, mkoani hapa kwa tuhuma za kumjeruhi kwa fimbo, mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 15, kinyume na Waraka wa elimu Na. 24, 2002.

Kamanda wa Polisi mkoani hupa, Janeth Magomi amesema tukio hilo lilitokea saa 4 asubuhi ya Jumatano ya Mei 14, 2025, shuleni hapo wakati wanafunzi wa darasa la saba wakiendelea na mtihani wa moko.

Akizungumza na Mwananchi jana Ijumaa, Mei 16, 2025, Kamanda Magomi amesema uchunguzi wa awali umebaini mwanafunzi alifutafuta karatasi ya majibu ya mtihani, baada ya kukosea jina la baba na kuichafua karatasi, ndipo mwalimu alipopatwa na hasira na kumshambulia kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha.

“Tuko kwenye upelelezi, kufahamu mwanafunzi alifanya nini mpaka aadhibiwe kwa kiasi hicho. Upelelezi wa awali ni kwamba mwanafunzi alifanya ujeuri kwa mwalimu, alifutafuta karatasi ya majibu akaichafua,” amesema Kamanda Magomi.

Kwa upande wake, Pauline Benedicto, mama mzazi wa mwanafunzi huyo amesema siku ya tukio alikuwa njiani akielekea shuleni kumpelekea chakula mwanaye aliyekuwa akifanya mtihani, ndipo alipokutana naye akilia na kueleza amepigwa na mwalimu.

Amesema baada ya kupokea maelezo ya mwanawe alimbeba kuelekea ofisi ya Serikali ya Kijiji, ambapo mwalimu Erick alipigiwa simu ya wito na viongozi wa Kijiji, lakini hakutokea kwa madai alikuwa akisimamia mitihani iliyokuwa inaendelea shuleni hapo.

Amesema baada ya kumpeleka hospitali aliongozana na viongozi wa Kijiji kwenda kwa mwalimu, ambaye alipohojiwa alikiri kutenda tukio hilo huku akiomba msamaha na kwamba zilikuwa ni hasira kutokana na kosa alilolitenda mwanafunzi wake.

“Nilipoenda hospitali nikaandikiwa dawa nikanunue dawa, sikuwa hata na hela, nikaongea na mwenye duka la dawa, niliporudi ofisi ya kijiji, viongozi wakasema natakiwa niende kwa mwalimu, kufika mwalimu akakubali kwamba alimpiga mtoto wangu,” amesema.

Mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Ngilimba (15) akiwa na majeraha ya fimbo mgongoni baada ya kushambuliwa kwa fimbo na Mwalimu mkuu Erick Ombeni, kwa madai ya kukosea jina la babu kwenye mtihani wa Moku. Picha na Amina Mbwambo

“Tulipofika kwa mwalimu akasema kweli mama mtoto huyu nilimpiga alikosea kidogo tu, ila kutokana na hasira niliyokuwa nayo nikampiga nikapitiliza, akasema mzazi naomba nisamehe, sitarudia tena,” amedai Pauline.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngilimba, Zuberi Mabula amedai baada ya mwalimu kukiri kosa, walimtaka kuishi na mtoto huyo ili ampatie matibabu, lakini aliwafukuza mama pamoja na mwanaye bila msaada wowote.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa mbunge wa Ushetu (CCM), Emmanuel Cherehani, Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama, Andrew Chatwanga aliwataka viongozi wa vijiji kuzingatia utaratibu wa kuitisha mikutano ya hadhara, ili kubaini na kutatua changamoto za wananchi kwa wakati.

“Mtoto ana makovu mgongoni kote, kichwani, eti amekosea jina la baba, hii sio sawa, viongozi wa vijiji fuateni utaratibu wa mikutano ya hadhara kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati, wananchi wanateseka wanakosa pa kusemea,” amesema.

Cherehani aliahidi kumsaidia matibabu mtoto huyo huku akiwataka walimu kuzingatia miongozo ya kazi zao kuepuka matendo ya fedheha kama hayo.

Waraka wa elimu Na. 24, 2002 unatoa mwongozo jinsi adhabu ya viboko inavyotolewa, kuwa inaweza kutolewa kwa utovu wa nidhamu uliokithiri au kwa makosa ya jinai yaliyotendeka shuleni au nje ya shule.

Adhabu itazingatia ukubwa wa kosa, umri, jinsi na afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja.

Vilevile, unaelekeza kuwa itatolewa na mwalimu mkuu au mwalimu mwingine atakayeteuliwa na mwalimu mkuu, kwa maandishi kila mara kosa linalostahili adhabu hii linapotendeka.

Mwanafunzi wa kike atapewa adhabu ya viboko na mwalimu wa kike, isipokuwa kama shule haina mwalimu wa kike.

Kila mara adhabu wa viboko inapotolewa iorodheshwe katika kitabu kilichotengwa kwa kusudi hilo, ikiwa ni pamoja na jina la mwanafunzi aliyepewa adhabu, kosa alilotenda, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu na mwalimu mkuu asaini.

Mwanafunzi au mzazi akikataa adhabu ya viboko atasimamishwa shule. Hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mwalimu yeyote atakayekiuka utaratibu wa adhabu ya viboko.

Aidha waraka huo unapiga marufuku mwalimu yeyote kuonekana na fimbo mkononi kwa lengo la kumwadhibu mwanafunzi.

Salma Omary, mkazi wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, akizungumza tukio hilo ameshauri vigezo vya kusomea ualimu viwe vigumu ili wapatikane walimu wenye wito na weledi wa kazi hiyo na kwa kuzingatia umri.

“Mimi naona pengine vigezo vya kusomea ualimu vimekuwa vyepesi, kabla ya kujiunga vyuoni hata kama wamekidhi vigezo basi iangaliwe namna ya kuwapa mtihani mwingine utakaotafsiri wito wa mwalimu tarajiwa, maana wengi ni kama hawana wito na kazi hii wanafanya bora liende,” amesema.

Mwalimu mmoja anayefundisha katika Shule ya Msingi Segese iliyopo Msalala wilayani Kahama amesema kinachosababisha hali hiyo ni kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili baadhi ya walimu kutokana na kutegemea mshahara pekee ambao hautoshelezi.

Ameishukuru Serikali kupandisha kima cha chini cha mshahara, lakini ameishauri kutekeleza kwa wakati masilahi mbalimbali ya walimu, ikiwa ni pamoja na kupandishwa madaraja na kuwapa motisha kwa kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi kwenye kazi zao.

“Haswa huku vijijini, huwezi kusema utafanya biashara, utaishi kwa kutegemea mshahara. Huwezi kufanya maendeleo, sasa wakati mwingine mwalimu anajikuta ugumu wa maisha unamfanya anakuwa na hasira sana, hata mwanafunzi akikosea kidogo adhabu inakuwa kubwa, si kwa makusudi ila saikolojia yake imezongwa na mawazo,” amesema mwalimu ambaye ameomba jina lake lisitajwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *