Dar es Salaam. Ingawa bado haijawa rasmi kwa kundi la waliokuwa makada wa Chadema linalounda G55 kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), yanayoendelea Masaki, Dar es Salaam, kunakofanyika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho, yanaongeza ithibati ya hilo.
Hilo linatokana na ukweli kwamba, katika eneo hilo, ukiacha wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chaumma, sehemu ya wanamuungano wa G55 wameingia ndani ya ukumbi wa mkutano, wakipokelewa kwa heshima.
Baadhi ya walioshuhudiwa wakiingia eneo hilo ni waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya Chadema katika uongozi uliopita, akiwemo Naibu Makatibu Wakuu wastaafu wa Zanzibar na Bara, Salum Mwalimu na Benson Kigaila.
Pia walikuwepo Mkurugenzi mstaafu wa Itifaki na Mambo ya Nje, John Mrema, Mwenyekiti mstaafu wa Kanda ya Kati, Devotha Minja na viongozi wengine.

Kundi la viongozi hao liliwasili katika eneo hilo saa 7:30 mchana, likitanguliwa na wanachama wengine waliojiondoa Chadema, akiwemo Khadija Mwago, Ntobi, Masoud Mambo, Henry Kilewo na Lembrone Mchome.
Walivyotinga ukumbini
Kundi la kina Mwalimu lilikuwa la mwisho kuingia baada ya wanasiasa wengine waliojiondoa Chadema kutangulia, wakizunguka huku na kule mithili ya watu wanaoratibu jambo fulani.

Licha ya kukaa pamoja katika eneo moja, kina Mwago hawakuwa watulivu, waliingia na kutoka huku wakiongea na simu muda mrefu zaidi.
Katika vikao hivyo vilivyosheheni ulinzi unaohusisha waliokuwa makamanda wa Chadema, Kamati Kuu ndiyo iliyoanza, huku wajumbe wa Halmashauri Kuu wakisubirishwa nje.
Baadaye saa 8:01 mchana, wajumbe wa Halmashauri Kuu waliitwa kwenda ukumbini, ikiwa ni dakika chache baada ya kundi la G55 kuingia ukumbini humo.
Tayari, Mwananchi Digital imeshaarifiwa kuwa, pamoja na mambo mengine, kuwakaribisha wanachama hao wapya ni sehemu ya ajenda zitakazojadiliwa katika kikao cha Halmashauri Kuu.

Hayo yameendelea wakati Ntobi na Mchome wakiwa nje ya ukumbi kabla ya baadaye kuitwa na kujumuika katika kikao hicho kinachoendelea hadi sasa.
Baada ya kutambulishwa katika kikao hicho, baadaye walitakiwa kutoka nje ya ukumbi kwa ajili ya kusubiri kuitwa tena ili waidhinishwe.
Kinachosubiriwa sasa ni taarifa rasmi ya iwapo sehemu ya wanamuungano hao wa G55 wamejiunga na Chaumma au vinginevyo, lakini tayari ‘wali wa kushiba umeshaonekana kwenye sahani’.