Mwalimu aliyetimuliwa kwa kughushi cheti kidato cha nne anavyopigania haki kortini

Musoma. Mahakama Kuu imempa kibali, mwalimu Kasoga Mangira aliyefukuzwa kazi baada ya kuitumikia Serikali kwa miaka 26, ili kufungua maombi ya mapitio ya mahakama kupinga kuachishwa kazi kwa madai ya kugushi cheti.

Uamuzi huo ambao umepatikana kwenye tovuti ya mahakama, ulitolewa Februari 12 na Jaji Marlin Komba wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma. Amepewa siku 30 kufungua maombi hayo.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo kilichoambatanishwa katika maombi hayo, Kasoga anadai hakutendewa haki alipoachishwa kazi na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) na uamuzi huo ukathibitishwa na Rais.

Kilichofanya aachishwe kazi mwaka 2022 ni madai ya kugushi cheti cha kumaliza elimu ya sekondari, licha ya kuwa alikuwa na vyeti vingine vya kitaaluma kutoka shule na vyuo mbalimbali vilivyomwezesha kuajiriwa mwaka 1996.

Anaeleza mwaka 1990, baada ya kuombwa na TSC, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), lilihakiki cheti chenye namba S0405/029 na kuthibitisha kuwa ni halisi, lakini mwaka 2022 akaitwa kwenye kamati ya nidhamu TSC.

Kulingana na kiapo chake, alipewa siku 15 za kujibu tuhuma za kugushi cheti. Anadai hakusikilizwa ipasavyo ili kumwezesha kuwasilisha ushahidi na hakupewa haki ya kumuuliza shahidi hata mmoja, maswali ya dodoso.

Anadai pamoja na kuwasilisha cheti hicho na uthibitisho wa uhakiki kutoka Necta, bado TSC na Rais hawakutilia maanani jambo hilo.

Anadai kuachishwa kwake kazi kumemletea ugumu wa maisha kwa kuwa alisitishiwa mshahara na masilahi mengine.

Ni kwa msingi huo, amewasilisha maombi mahakamani ya kupewa kibali ili kufungua maombi kupinga uamuzi wa TSC na Rais.

Majibu ya Serikali

Wajibu maombi katika shauri hilo ambao ni Katibu Mtendaji wa TSC kama mjibu maombi wa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) (mjibu maombi wa pili) walipinga madai hayo.

Katika kiapo cha pamoja, wajibu maombi walidai mwombaji katika jalada lake binafsi alikutwa akimiliki vyeti viwili vya kumaliza kidato cha nne, ambavyo Necta ilikuwa imevithibitisha kuwa vimeghushiwa.

Walieleza mleta maombi alipewa haki ya kusikilizwa kupitia TSC ambako kwa ujumla walibishania kile kinachoombwa na mwombaji, hivyo hakiwezi kubadilisha chochote katika uamuzi uliokuwa umefikiwa na TSC mwaka 2022.

Uamuzi wa jaji

Katika uamuzi wake, Jaji Komba alisema ni wajibu wa Mahakama kupima kama mwombaji amejenga hoja zinazojadilika kwa kuwa ana nia ya kuomba mapitio ya mahakama kupinga uamuzi wa TSC.

Jaji alisema maombi ya mapitio ya mahakama ni aina ya kesi zinazoangukia katika sheria za utawala ambazo zinahusika na matendo ya kiutawala na maamuzi ya mamlaka au vyombo vya kisheria kama TSC.

“Katika shauri lililopo mbele yangu, mwombaji ana nia ya kupinga uamuzi uliofanywa na TSC na Rais. Ofisi ya Rais ni ofisi ya umma na maamuzi inayoyafanya ni ya kiutawala. Naona shauri linafaa kufunguliwa kama mapitio ya mahakama.

“Hata hivyo, katika kutoa kibali cha kufungua maombi hayo ni lazima mwombaji akidhi masharti ambayo yamewekwa na sheria ambayo yamewahi kufanyiwa uchambuzi katika shauri la rufaa la Emma Bayo dhidi ya Waziri wa Kazi,” alisema.

Masharti yaliyowekwa ni pamoja na mahakama ijiridhidhe mwombaji ana kesi yenye mashiko, kama yuko ndani ya ukomo wa miezi sita ya kupinga uamuzi huo na kama ameonyesha masilahi ya kutosha kuruhusiwa kufungua maombi hayo.

Jaji alisema katika shauri lililo mbele yake, wajibu maombi kupitia mawasilisho yao walikubali kuwa mleta maombi ana hoja za msingi kwa kuwa analalamikia haki ya kusikilizwa.

“Ninafahamu maombi ya kupewa kibali na mahakama ni mchakato wenye lengo la kuiwezesha mahakama kuondoa maombi yasiyo na mashiko ambayo yatafanya ionekane kama ni matumizi mabaya ya mchakato wa kimahakama,” alisema.

Kutokana na uchambuzi alioufanya na mawasilisho ya wajibu maombi, jaji alisema anaona kuna hoja za msingi za kushughulikiwa hasa malalamiko ya kutopewa haki ya kusikilizwa, hivyo akatoa siku 30 kwa mwombaji kuwasilisha maombi.