Mwakinyo ashikiliwa kituo cha Polisi Tanga, sababu yatajwa

Bondia wa ngumi za kulipwa nchini na bingwa wa mkanda wa WBO Afrika katika uzani wa middle, Hassan Mwakinyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga akituhumiwa kumshambulia mtu anayedaiwa kuingia katika eneo lake bila ya ridhaa yake.

Mwakinyo anashikiliwa na jeshi hilo tangu jana Alhamisi katika Kituo cha Chumbageni kutokana sakata hilo, huku mtu aliyemshambulia akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo Tanga.

Chanzo cha kuaminika kimelieza Mwananchi kuwa sababu kubwa ya bondia huyo kushikiliwa na jeshi hilo ni kutokana na madai ya kumshambulia mtu huyo na kumsababishia majeraha makubwa mwilini.

Mwananchi limemtafuta Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Maket Msangi ambaye amekiri kuwa wanamshikilia bondia huyo maarufu nchini.

“Sisi tunamshikilia Hassan Mwakinyo, hatumshikilii bondia. Hakuna shida ila ana tuhuma za kumshambulia mtu ambaye inasemekana alipita maeneo ya nyumbani kwake na kujaribu kuingia kwa namna ya mazingira ambayo inadaiwa ni kwa nia ya kutenda kosa, kwa hiyo akamkamata,” amesema Msangi.

“Wakati tunapewa taarifa alikuwa amemkamata, polisi tulienda kwa ajili ya kumchukua mtuhumiwa lakini alikuwa kidogo ana majeraha, tukampeleka akapate huduma ya kwanza Bombo kwa hivyo tunamshikilia kutokana na kumkuta mtuhumiwa kidogo ana majeraha, Tunaendelea kumhoji Mwakinyo kwa nini mpaka akajeruhiwa hivyo.

“Hivyo elewa kwamba tunamshikilia kwa sababu hiyo, tutafikisha suala (hilo) ofisi ya mashtaka kwa ajili ya kutafsiri sheria na kama kuna tatizo, ushahidi unathibitisha kosa basi hatua nyingine stahiki zitachukuliwa.”