Mwakilishi wa Algeria UN: Algiers inalaani vikali shambulizi la Israel dhidi ya Iran

Balozi na mwakilishi wa Algeria katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amelaani vikali mashambulizi ya hivi majuzi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran.

Ammar Bin Jame amesema: “Hii leo tunashuhudia mzozo wa kikanda ambao umeathiri eneo zima la Magharibi mwa Asia na hata ulimwengu mzima.”

Balozi Ammar Bin Jame amesema: Baadhi ya wawakilishi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hawajali kuhusu yanayojiri. Amesisitiza kuwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran yanakiuka sheria za kimataifa. “Tunaunga mkono Iran na tunalitambua shambulio la Israel kama ukiukaji wa uhuru na mamlaka ya kujitawala ya Iran”, amesisitiza balozi na mwakilishi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa.

Balozi Bin Jame amesema jamii ya kimataifa ina wajibu wa kukomesha jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel.

Usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita utawala wa Kizayuni wa Israel ulishambulia vituo kadhaa vya kijeshi vya Iran na kuua maafisa wanne wa Jeshi na raia mmoja.

Iran imesisitiza kuwa haitaki vita lakini haitaacha haki yake ya kutoa jibu linalofaa na thabiti kwa kitendo kwa uchokkozi huo wa Israel.