Mwaka wa tatu huu Tems anaishi London

Dar es Salaam. Mshindi wa Grammy na mkali wa Afrobeats kutokea Nigeria, Tems amesema huu ni mwaka wa tatu sasa anaishi London, Uingereza kwa ajili ya shughuli zake za kimuziki pamoja na mambo yake mengine binafsi kama familia.

Hata hivyo, Tems aliyetikisa na wimbo, Essence (2020) alioshirikiana na Wizkid, amesema licha ya kuhamia London bado Lagos, Nigeria ni nyumbani kwao na mara kwa mara huwa anaenda.

Tems, mshindi wa tuzo tatu za BET, amefunguka hayo wiki hii katika mahojiano yake na Jarida na Billboard ambapo pia amezungumzia maisha yake ya umaarufu

“Nimeishi London kwa takribani miaka mitatu sasa. Familia yangu ilihamia hapa nilipokuwa mtoto, Baba yangu bado anaishi hapa. Ila kwa kweli, nililelewa Lagos, hivyo sikukaa hapa kwa muda mrefu sana nilipokuwa mtoto,” alisema na kuongeza.

“Kwa hiyo ni wazi Lagos bado naichukuliwa kama nyumbani kwetu,” alisema Tems ambaye anaendelea kufanya vizuri na albamu yake ya kwanza, Born in the Wild (2024).

Ikumbukwe Tems alizaliwa Juni 11, 1995 huko Lagos, na muda mfupi baadaye familia yake ilihamia Uingereza maana baba yake ni raia wa huko, akiwa na umri wa miaka mitano wazazi wake waliachana kwa talaka, hivyo akareja Nigeria na Mama yake.

Staa huyu alianza kuvuma Nigeria na Afrika baada ya kutoa EP yake ya pili, If Orange Was a Place (2021) yenye nyimbo kali kama ‘Free Mind’ ulioshika nafasi ya kwanza chati za Billboard U.S. Afrobeats Songs na Bubbling Under Hot 100.

Katika hatua nyingine, Tems alipoulizwa na Billboard umewezaje kukabiliana na maisha ya umaarufu huku akiendelea kufanya vizuri katika muziki, alisema ni kukaa mbali na mambo anayoona si sawa kisha kuwekeza nguvu kubwa katika kazi yake.  

“Angalau nilipoanza, kuna mambo mengi ambayo sikuwa na raha nayo. Nilikuwa na wasiwasi sana kwa mambo mengi, kwa hivyo kila kitu kilikuwa kibaya. Ninapenda muziki tu, siku zote nimekuwa nikizingatia sanaa yangu na kuandaa muziki tu,” amesema.

“Lakini ninapata furaha, unajua; ninakuwa na utulivu na kuwa na wakati wangu mwenyewe, na mimi huweka maisha yangu ya faragha, kama vile maisha yangu ya kibinafsi, hivyo nayatenganisha na maisha yangu ya umaarufu,” alisema Tems.

Utakumbuka katika tuzo za 67 za Grammy 2025, Tems alishinda katika kipengele kipya ambacho ni maalumu kwa muziki wa Afrika cha ‘Best African Music Performance’ kupitia wimbo wake, Love Me Jeje (2024).

Hii ilikuwa tuzo ya kwanza ya Grammy kwa Tems kushinda kupitia kazi yake binafsi kwani aliyoshinda 2023 katika kipengele cha Best Melodic Rap Performance, ni kutokana na kushirikishwa katika wimbo wa Future, Wait For U (2022) ambao ndio ulioshinda.

Hivyo, kufuatia ushindi huu wa Grammy 2025, Tems aliweka rekodi kadhaa ikiwemo ya msanii wa kwanza wa kike Nigeria kushinda Grammy kupitia kazi yake, na wa pili baada ya Burna Boy kushinda 2021 kupitia albamu yake ya tano, Twice As Tall (2020).
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *