Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kutunza amani ya nchi bila kuruhusu ushawishi wa aina yoyote wa kuivunja.
Amesema wale wanaotamani kuvuruga amani wanapaswa kutafakari hali ya baadhi ya mataifa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na duniani, ambako wananchi wanateseka kutokana na ukosefu wa utulivu, ikiwemo vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Februari 9, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene aliyemwakilisha Rais Samia, wakati wa ibada ya kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.

Ibada hiyo imefanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli Kati.
Kwa niaba ya Rais, Waziri Simbachawene amesema amani na utulivu ni msingi wa maendeleo ya taifa, hivyo kutoweka kwake kunaweza kuhatarisha mafanikio yaliyopatikana kwa zaidi ya miaka 60 ya uhuru.
“Amani na utulivu ni msingi wa ustawi wa nchi. Bila amani, hatuwezi kufanya lolote. Niko hapa kwa niaba ya Rais, ambaye amenituma kusisitiza umuhimu wa kulinda amani kwa ajili ya maendeleo yetu,” amesema Simbachawene.
Amesema; “Tuangalie mataifa jirani ambayo yalijijenga kwa muda mrefu kwa kutumia rasilimali nyingi walizonazo, lakini machafuko yameharibu kila kitu walichokijenga. Leo wamesalia na kilio tu.”
Aidha, waziri huyo amesema Lowassa alikuwa miongoni mwa watu walioweka misingi ya amani nchini, hivyo ni muhimu kuendelea kumuenzi kwa mchango wake mkubwa kwa Taifa.
Naye Regina Lowassa mjane wa Lowassa akitoa shukrani wakati wa ibada hiyo, mbali ya kuwashuru watu wote waliofika kanisani hapo, amesema ilikuwa vigumu kuzoea hali ya kuondokewa na mumewe, lakini kadiri sikun zinavyozidi kwenda anaamini ni kweli mumewe amefariki dunia.
“Tangu mume wangu afariki, Mungu amekuwa akiniongoza na kunifariji kwa kuniweka karibu na watu wa makundi mbalimbali, wakiwamo viongozi wa dini, mila, siasa na jamii,” amesema Regina.
Hata hivyo, anasema; “Nina hakika kama mume wangu alifariki akiwa na hofu ya kuacha familia, leo hii akipewa dakika moja afufuke na aone umati huu uliokusanyika kutufariji, atarudi kulala kwa amani akijua kuwa familia yake iko salama.”
Kwa upande wake, Frederick Lowassa, mmoja wa watoto wa Lowassa, amesema kumbukizi hiyo imelenga kumpa baba yao heshima na kuenzi kazi zake.
Frederick ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, amesema ataendelea kuwatumikia wananchi wa Monduli kwa kadri atakavyopata fursa ya kufanya hivyo.
“Sitaweza kutimiza kila kitu alichofanya baba yangu, lakini nitajitahidi kufuata nyayo zake kwa kadri nitakavyowezeshwa na Mungu na kwa ridhaa ya wananchi,” amesema.
Akihubiri katika ibada hiyo iliyoongozwa na Mchungaji Ezekiel Megiroo, Askofu mstaafu Solomon Masangwa amesisitiza umuhimu wa nchi kujitegemea ili kuepuka utegemezi wa misaada ya nje, hasa pale inapositishwa.
“Wakati tunamuenzi Lowassa, tukumbuke juhudi zake za kuhakikisha taifa linajitegemea. Leo tungekuwa tumepiga hatua kubwa, tusingeyumba kwa uamuzi wa Marekani wa kusitisha misaada,” amesema Askofu Masangwa.
Baada ya ibada, mamia ya wananchi wameelekea nyumbani kwa Lowassa kwa chakula cha pamoja na imeelezwa kuwa zaidi ya ng’ombe 30 na mbuzi 50 wamechinjwa kwa ajili ya misa hiyo ya shukrani.