Lakini sasa wanakabiliwa na mtazamo tofauti kuhusu njia gani ya kufuata kuelekea mbele.
Kwa mujibu wa wachambuzi, maandamano hayo yaliyofahamika kama maandamano ya kizazi cha Gen Z yalijitokeza kwa ghafla, bila uongozi rasmi, na kugeuka kuwa vuguvugu la aina yake katika historia ya Kenya.
Yalichochewa na mswada wa fedha uliopendekeza ongezeko kubwa la kodi, hali ambayo iliwaumiza zaidi wananchi wa kipato cha chini, huku kukiwa na kashfa za mara kwa mara za ufisadi serikalini. Takribani asilimia 40 ya Wakenya wanaishi katika umasikini.
Msako na vifo baada ya maandamano
Wimbi la maandamano hayo lilipamba moto hadi kilele chake cha Juni 25,ambapo maelfu ya waandamanaji walivamia bunge wakati wabunge wakijadili mswada huo. Hatimaye, shinikizo hilo lilimlazimisha Rais William Ruto kuondoa mswada huo.
Hata hivyo, wiki zilizofuata zilishuhudia msako mkali wa polisi uliosababisha vifo vya watu 60 na wengine wengi kuwekwa kizuizini kinyume na sheria. Kwa vijana wengi, hii ilikuwa ishara ya mfumo wa utawala usiotaka mabadiliko.
Wachambuzi wanabaini kuwa maandamano hayo yalikuwa hatua mpya ya uanaharakati nchini Kenya, ambapo vijana walivuuka mipaka ya kikabila na kijiografia iliyokuwa ikitawala siasa kwa muda mrefu, na badala yake kuzingatia ajenda za sera.
Lakini sasa kuna mgawanyiko ndani ya vuguvugu hilo. Wakati baadhi ya wanaharakati kama Hanifa Adan wameendelea kushiriki maandamano ya kupigania haki za wanawake na kupinga ukatili wa polisi, wengine wameamua kufuata njia tofauti.
Miongoni mwa waliobadili mwelekeo ni Kasmuel McOure, kijana mwenye umri wa miaka 27 aliyepata umaarufu kupitia hotuba zake kali wakati wa maandamano.
Hivi sasa amejiunga na chama cha upinzani cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, ambaye kwa sasa ana ushirikiano na serikali.
McOure anasema kwamba kujiunga kwake na siasa rasmi ni hatua ya kimkakati, akiongeza kuwa vijana wanapaswa kushika madaraka ya kisiasa badala ya kubaki waandamanaji wasio na mwelekeo.
“Sababu yangu ya kujiunga na ODM na kuachana na vuguvugu la maandamano ni kwamba niliona kwamba watu wengi waliokuwa wakijiita viongozi humo walikuwa wakichochea tu kwa ajili ya kufanya usumbufu,” alisema McOure
Wimbi la vijana wanaotaka kuwania uongozi
McOure anasisitiza kuwa harakati ya Gen Z ilikuwa imekosa mpangilio thabiti wa kuleta mabadiliko halisi. Hata hivyo, hana uhakika kama atagombea ubunge mwaka 2027, lakini anasisitiza kuwa vijana hawana budi kujitokeza na kuchukua nafasi katika uongozi.
Kwa upande wake, Hanifa Adan anakubaliana kwamba ni muhimu vijana kushika hatamu za uongozi, lakini bila kukubaliana na mfumo uliopo ambao mara nyingi umejikita katika ufisadi.
Anasisitiza kuwa kuna kizazi kipya cha viongozi wachanga wanaojitayarisha kuwania nyadhifa mbalimbali bila kujiunga na vyama vikuu viwili vyenye historia ya ufisadi.
Kwa Adan, tofauti ndani ya vuguvugu la vijana ni jambo la kawaida na linaonyesha nguvu ya utofauti wa mawazo.
Anaongeza kuwa vijana waliopambana na gesi ya machozi, waliopanga huduma za matibabu na kampeni za mtandaoni, sasa wanaelekeza nguvu hizo katika kutafuta nafasi za kuchaguliwa ili kuleta mabadiliko ya kweli.