Mwaikimba atia neno ubora wa wachezaji Ligi Kuu

STRAIKA wa zamani wa Yanga na Azam FC, Gaudence Mwaikimba amesema akiitazama Ligi Kuu Bara kwa sasa kilichoongezeka ni uwekezaji, lakini kuhusu ufundi wa wachezaji uwanjani haoni vipaji halisi kama ilivyokuwa zamani.

Aliifafanua kauli yake kwamba kilichotawala kwa sasa ni mbinu za makocha zinapofeli timu inakuwa ngumu kupata matokeo mazuri huku akisema mpira anaouona kwa wachezaji ni wa maelekezo ambayo yanaficha uhalisia wa vipaji vyao.

“Wachezaji wana uwezo mkubwa ila wakicheza kinachoonekana ni maelekezo ya makocha ama mbinu, kwa kifupi makocha wanacheza zaidi ya wachezaji.

“Mfano mzuri hadi sasa raundi ya 23 kwenye Ligi Kuu anayeongoza kwa mabao ni Jean Charles Ahoua wa Simba amefunga 12, ila kipindi cha nyuma ulikuwa ukimtaja John Bocco au Kipre Tchetche wangekuwa na mabao 17 hadi 18 kipindi kama hiki kwani walikuwa wanacheza kwa kiwango kikubwa.

“Baadhi ya vipaji vikubwa kuanzia miaka 2016 kurudi nyuma vilivyokuwa Ligi Kuu upande wa washambuliaji ni Bocco, Boniface Ambani, viungo walikuwepo Athuman Idd ‘Chuji’ marehemu Godfrey Bonny ‘Ndanje’ hao ni baadhi tu, lakini walikuwa na vipaji vikubwa sana na wakiwepo uwanjani unaona uwezo wao wa kuamua matokeo na kuzichezesha timu zao,” alisema Mwaikimba huku akisisitiza Jonathan Sowah wa Singida Black Stars kama angeingia mwanzoni mwa msimu anaamini angekuwa na idadi kubwa ya mabao kulinganisha na sasa akiwa nayo saba kwenye mechi saba.

Mbali na hilo, anakumbushia enzi zake na misimu ambayo iliyobaki katika kumbukumbu zake ni 2005/06 akiwa Ashanti United alimaliza na mabao 15 huku 2011/12 wakati yupo Kagera Sugar alimaliza na mabao 14 akiwa nafasi ya pili katika orodha ya ufungaji bora.

“Nikizungumzia kwenye nafasi yangu hiyo ilikuwa misimu mizuri kwangu kwani yote miwili nilimaliza mfungaji namba mbili,” alisema Mwaikimba anayesimamia timu ya New Fighters inayocheza Ligi Daraja la Tatu, Ipinda mkoani Mbeya.

Mwaka jana timu hiyo ilifika hatua ya fainali katika mashindano ya mkoa na kupoteza mbele ya Tukuyu Stars huku msimu huu ikiishia nusu fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *