Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi amesimulia kile ambacho walikuwa wakikifanya siku nzima na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima kabla ya kushambuliwa.
Padri Kitima amelazwa hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na kitu butu kichwani usiku wa jana Jumatano, Aprili 30, 2025. Shambulio hilo lilitokea eneo la Kurasini Temeke, Dar es Salaam, zilipo ofisi za TEC Makao Makuu.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima
Viongozi mbalimbali wa Kanisa Katoliki, waumini na wanasheria wamejitokeza kwa wingi kumjulia hali Padri Kitima aliyelazwa Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu wa Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wanamshikilia Rauli Mahabi, mkazi wa Kurasini jijini Dar es Salaam akituhumiwa kuhusika na tukio hilo lililotokea saa 4:15 usiku, baada ya kudaiwa kumshambulia Kitima alipokwenda maliwatoni pembeni ya kantini, alipokuwa akipata kinywaji kuanzia saa 1 jioni.
Kamanda Muliro amesema Padri Kitima alishambuliwa kichwani na kitu butu na watu wawili. Uchunguzi wa kina unaendelea ili hatua kali na haraka zichukuliwe kwa wahusika.
Leo Alhamisi, Mei 1, 2025, Mwananchi imeshuhudia kundi la mapadri, masista, waumini na wanasheria wakiingia wodini alikolazwa kiongozi huyo kumjulia hali.
Nje ya hospitali hiyo, Mwananchi limezungumza na Mwabukusi ambaye mbali na kuzungumzia maendeleo ya Padri Kitima lakini amegusia kile walichokuwa wakikifanya jana Jumatano na kiongozi huyo kabla ya kushambuliwa.
“Tulikuwa na programu pale siku nzima ofisini kwake jana ambayo tuliiendesha mimi na yeye ya uwezeshaji kuzungumzia masuala ya reforms (mabadiliko) ndogo za uchaguzi, tulianza asubuhi hadi jioni kwenye saa 12 hivi.”
“Kwa sababu wenzetu walikuwa na kazi ya majumuisho ili isambazwe moja kwa moja kwa wadau hivyo tulimuacha Padri Kitima, mimi nikawahi sehemu niliyofikia kwa sababu nilifikia eneo jingine, usiku ndio nikasikia kashambuliwa,” amesema.
Mwabukusi amesema kwa kazi ambayo viongozi hao walikuwa wakifanya hakukuwa na utaratibu wowote wa kunywa kama polisi wanavyosema kwani kwa kuwa kazi ambayo viongozi walikuwa wakifanya ilipaswa kukamilika jana na kuanza kusambazwa leo kwa wadau.
“Mimi najua kazi iliyokuwa inafanyika, ile kazi siyo ya kunywa, ilikuwa kazi ya kuandika na ilikuwa ifanyiwe kazi leo na wala si kazi ya kunywa,” amesema Mwambukusi.
Mwambukusi amedai shambulio dhidi ya Padri Kitima lililenga kuondoa uhai wake kutokana na sehemu aliyojeruhiwa.
“Mhusika kalenga mauaji, Padri Kitima kashonwa kuna taarifa zimetoka kwamba anadai kuumizwa kauli hii ni ya kinyama na imenisikitisha, Watanzania tumuombee Padri kaumizwa na siyo inadaiwa kaumizwa ni kaumizwa na mpigaji alitaka kuua,” amedai.
Chadema walaani
Kutokana na tukio hilo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinalaani kwa nguvu zote shambulio la kinyama dhidi ya Padri Kitima.
Taarifa kwa umma ya Chadema iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia imesema: “Tukio hili linatisha na linaashiria mazingira hatarishi kwa viongozi wa dini na watetezi wa haki wanaoibua hoja za msingi kuhusu mwelekeo wa taifa, ikiwemo mabadiliko ya sheria na kanuni za uchaguzi.”
“Tunazitaka mamlaka husika zichukue hatua za haraka kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika wa tukio hili. Vilevile, Serikali itimize wajibu wake wa kulinda usalama wa viongozi wa dini, wanaharakati na wananchi wote, kwani vitendo vya uvamizi na watu kupotea vimeanza kuzoeleka kwa namna ya kuitisha,” amesema Brenda.
“Chadema inatoa pole kwa Padri Kitima, familia yake na Baraza la Maaskofu Katoliki kwa mshtuko na madhila yaliyotokea. Tunaungana nao katika kusisitiza haja ya kulinda misingi ya utu, usalama na uhuru wa kujieleza.”