Mvua zazua kizaazaa

Dar/Mikoani. Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zimeanza kuleta athari, huku wananchi wanaoishi maeneo hatarishi wakiaswa kuhama.

Wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam daraja la muda linalounganisha Bonyokwa na Kinyerezi limekatika, huko wanafunzi watano wakizingirwa na maji walipokuwa wakifua nguo mtoni wilayani Morogoro. 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika taarifa kuhusu mwenendo wa mvua za masika (Machi hadi Mei) 2025 ilisema mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya pwani ya kaskazini, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na ukanda wa Ziwa Victoria (mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na magharibi mwa mikoa ya Simiyu na Mara).

TMA ilisema mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki na mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu.

Mamlaka ilisema mvua za masika zilitarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Machi, 2025 katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria na pwani ya kaskazini na katika wiki ya pili na ya tatu ya Machi, 2025 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki. Ongezeko la mvua linatarajiwa kuwa Aprili, 2025

Pia ilitoa ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa.

Mamlaka ilitaja athari zinazotarajiwa ni vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka, hivyo kuongeza hatari ya mafuriko hususan katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko. Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji.

Hali ya Dar es Salaam

Mvua iliyonyesha jana (Machi 27) imekata daraja la muda linalounganisha maeneo ya Bonyokwa na Kinyerezi, hivyo kusababisha adha ya usafiri.

Daraja hilo lilitengenezwa baada ya lile awali kubomolewa na wakandarasi wanaoendelea na ujenzi wa barabara.

Mkazi wa Bonyokwa, Sara Philimon amesema: “Sijaenda kazini leo (Machi 28) kwa sababu daraja limekatika. Si mimi pekee, hata wanafunzi wameshindwa kwenda shule. Wengine wanalazimika kupelekwa na wazazi wao. Tunaomba Serikali itusaidie kurudisha hali ya kawaida, maana tunateseka,” amesema.

Samaduni Mlimbwa, mkazi wa Bonyokwa Kisiwani, amesema walishatoa ushauri kwa mkandarasi kabla ya kujengwa daraja la muda lakini ushauri wao haukuzingatiwa.

“Tulieleza daraja la muda wanaloweka halitaweza kusaidia kwa sababu maji yanapita kwa wingi na njia waliyoweka ni ndogo. Pia, mvua mara nyingi huja na takataka kama miti na majani. Lakini hawakutusikiliza, na sasa hali ndiyo hii,” amesema.

Katika hatua nyingine, wakazi wa Kigogo Mbuyuni wamesema kusafishwa kwa Mto Msimbazi kumewezesha maji kupita pasipo wao kuathiriwa.

Mkazi wa Kigogo, Asha Shukurani amesema baada ya mto kusafishwa na mchanga kuondolewa maji hayaathiri nyumba zao.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kigogo Mbuyuni, Kata ya Kigogo, Abdallah Mkuja, amesema usafishaji wa mto umepunguza kwa kiasi kikubwa adha ya mafuriko.

“Tunashukuru kwamba tangu mvua zimeanza kunyesha maji yanapita vizuri baada ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kusafisha na kuondoa miti na magogo yaliyokuwa yamenasa kwenye matundu ya daraja katika Barabara ya Kawawa,” amesema.

Mkoani Morogoro

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabani Marugujo amesema mvua iliyoanza kunyesha Machi 27 saa 11:00 jioni imesababisha wanafunzi watano wa Shule ya Sekondari ya Jabal Hilla Islamic iliyopo Manispaa ya Morogoro wazingirwe na maji walipokuwa wakifua nguo kando mwa Mto Morogoro.

Kamanda Marugujo amewataka wanafunzi waliookolewa ni wa kidato cha kwanza Joel Aloyce (14) na Sadrudin Abdallah (13) na wa kidato cha sita Mohamed Ally (21), Yahaya Hakimu (21) na Abdallah Shafii (21).

“Taarifa za wanafunzi hao kuzingirwa na maji tulizipata baada ya msamaria wema kufika kwenye ofisi zetu. Askari walikwenda eneo la tukio na kuwaokoa kabla hawajapata madhara,” amesema.

Ametoa tahadhari kwa wananchi kutofanya shughuli zozote kando mwa mito hasa katika kipindi hiki cha mvua.

“Mvua hizi zilianza mapema wiki hii kwa kunyesha kidogo kidogo isipokuwa kuanzia (Machi 27) ndipo imenyesha kubwa, mpaka sasa bado hatujapata taarifa za mafuriko wala madhara makubwa ila kama mvua hii itaendelea mpaka kesho upo uwezekano wa kutokea mafuriko hasa katika maeneo yale ambayo yapo mabondeni,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amesema mvua zinazonyesha hazijaleta madhara wilayai humo licha ya kuwepo baadhi ya maeneo kupitiwa na maji kutokana na mitaro kuziba.

Amewataka wananchi wachukue tahadhari, wazazi wawe makini na watoto wao kwa kutowaruhusu kucheza kando mwa madimbwi, mito na makorongo.

Pia walimu wametakiwa kuwa makini na wanafunzi wanapokuwa shuleni.

Maagizo Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimajaro, Nurdin Babu amewataka wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuondoka mara moja ili kuepuka majanga.

Babu amesema baadhi ya maeneo yamekuwa yakiathiriwa na mvua, hivyo ni lazima wananchi wachukue tahadhari mapema.

“Niwatake wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, kuhakikisha wananchi walioko kwenye maeneo hatarishi wanatoka na hasa nyakati hizi za mvua,” amesema.

Pi amezitaka mamlaka husika kuweka mikakati ya kuzibua mifereji na madaraja yaliyoziba na kujaa tope ili kuruhusu maji kupita.

“Nizielekeze mamlaka zinazohusika na barabara kuhakikisha zinakarabatiwa na zinapitika, hasa kipindi hiki cha mvua ili kuendelea kuwa na uhakika wa huduma ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi nyakati zote,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Dionis Myinga amesema tayari wametoa elimu kwa wananchi walioko maeneo hatarishi kuondoka na wameanza kuhama.

Ameyataja maeneo yenye changamoto kuwa Sanya Stesheni na Rundugai.

Baadhi ya wananchi wa maeneo ya Kata ya Mji Mpya wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwatafutia maeneo mengine mbadala kwa kuwa hawana pa kwenda.

Hadija Juma, mkazi wa Kwakomba ameomba kutafutiwa eneo mbadala ili akaishi na familia kwa kuwa hana pa kwenda.

“Ni sawa tupo kwenye maeneo hatarishi na hata mwaka huu, maeneo yetu yalipatwa na mafuriko na baadhi ya nyumba kusombwa na maji na watu kupoteza maisha, hivyo Serikali iangalie namna ya kutusaidia maana hatuna pa kwenda,” amesema kauli iliyoungwa mkono na Elinihaki Mbwambo, mkazi wa Kahe.

Imeandikwa na Devotha Kihwelo (Dar), Hamida Shariff (Morogoro), Florah Temba na Janeth Joseph (Moshi)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *