Mvua za masika kuhamisha waliojenga mabondeni Zanzibar

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito kwa wananchi wanaoishi mabondeni kujiandaa kuhama mapema na kusafisha mazingira yanayowazunguka, na kutokuchafua miundombinu inayopitisha maji ya mvua.

Pia, ameagiza mabaraza ya manispaa, mabaraza ya miji na halmashauri za wilaya kuhakikisha wanadumisha usafi katika kipindi chote kabla ya mvua na wakati wa mvua za masika ili kuepuka maradhi ya milipuko.

Abdulla amebainisha hayo leo Februari 28,2025 aalipokuwa akiahirisha mkutano wa 18 wa Baraza la 10 la Wawakilishi, katika Ukumbi wa baraza hilo Chukwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kanda ya Zanzibar mvua za masika kwa mwaka 2025 zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Machi na kumalizika wiki ya mwisho ya Mei.

Amesema, mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini na zitakuwa za kawaida au zitapungua kidogo hivyo kuna uwezekano wa kutokea matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika baadhi ya siku, hivyo kuleta madhara katika maisha ya watu na mali zao.

“Kwa muktadha huo, natoa wito kwa wananchi wanaoishi mabondeni kujiandaa kuhama mapema kusafisha mazingira yanayotuzunguka pamoja na kutochafua na kuharibu miundombinu inayopitisha maji ya mvua katika maeneo yao,” amesema. 

Pia, amesema Serikali inaendelea kuimarisha sekta muhimu ya afya kwa kuwajali wananchi wanaoishi katika visiwa vidogovidogo vinavyozunguka visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuwapelekea boti maalumu za kubebea wagonjwa, wajawazito na huduma za dharura.

Abdulla amesema, Serikali inaahidi kuifanyia kazi ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na kamati kwa kuhakikisha ufanisi wa utendaji kazi wa Serikali unaleta matokeo chanya.

Amesema, baraza hilo limepitisha miswada ya sheria ikiwemo wa sheria ya kufuta sheria ya baraza la udhibiti wa mfumo wa utoaji leseni za biashara, namba 13 ya mwaka 2013 na kutunga sheria ya udhibiti na usimamizi wa utoaji wa leseni za biashara Zanzibar.

Pia imepitisha muswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya ununuzi na uondoaji wa mali za umma namba 11 ya mwaka 2016 na kutunga sheria ya ununuzi wa umma na kuweka masharti bora ya kusimamia na kudhibiti ununuzi wa umma.

Hemed amesema, kupitishwa kwa miswada hiyo miwili Serikali ina matumaini makubwa ya kuongeza tija na ufanisi katika kutoa huduma bora za utoaji leseni kwa wafanyabiashara, pamoja na masuala ya usimamizi na kudhibiti ununuzi wa umma kwa masilahi ya nchi.

Amesema, Serikali inaendelea na azma ya kuimarisha miundombinu mbalimbali nchini ili kuwawekea mazingira bora wananchi ikiwamo kubuni vyanzo mbalimbali vya upatikanaji wa fedha akitolea mfano kuanzishwa kwa Zanzibar SUKUK.

Zanzibar SUKUK ni uwekezaji wa hati fungani inayofuata maadili na miongozo ya sharia ya Kiislam.

Amesema nchi nyingi zimekuwa zikitumia utaratibu huo katika kuwaletea maendeleo wananchi wao na kuimarisha miundombinu ya nchi.