Mechi ya ufunguzi wa uwanja mpya wa Singida Black Stars baina ya timu hiyo na Yanga, imeishia katika dakika ya 57 kutokana na mvua kubwa kunyesha iliyosababisha mchezo huo kutoendelea.
Timu hizo mbili zimekubaliana kutoendelea na mechi hiyo muda mfupi baada ya Singida Black Stars kusawazisha bao kupitia kwa Marouf Tchakei.
Kabla ya hapo, Jonathan Ikangalombo aliandika historia ya kuwa mfungaji wa kwanza wa bao katika uwanja huo.

Ikangalombo alifunga bao hilo katika dakika ya 19, baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Singida Black Stars na kumalizia kwa ustadi mkubwa. Bao hilo lilikuwa la kiufundi, likionyesha ubora wake katika eneo la ushambuliaji.
Mchezo huo ulianza kwa kasi, huku pande zote zikishambuliana kwa zamu. Singida Black Stars walionekana kupania kulinda heshima yao nyumbani, lakini walikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Yanga, ambao walionyesha umahiri wao uwanjani.

Hali ya hewa ilianza kubadilika mwanzoni mwa kipindi cha pili, ambapo mvua ilianza kunyesha taratibu. Mashabiki waliendelea kushuhudia mchezo kwa matumaini kuwa mvua hiyo haingeathiri mchezo.
Dakika chache baadaye, mvua hiyo iliongezeka kasi na kuambatana na upepo mkali. Hali hiyo iliwafanya mashabiki wa timu zote kukimbilia maeneo ya kujikinga, huku wachezaji wakijitahidi kuendelea na mchezo.

Licha ya juhudi za waamuzi kujaribu kuruhusu mchezo kuendelea, hali ya hewa ilizidi kuwa mbaya zaidi. Hatimaye, katika dakika ya 57, mwamuzi alilazimika kusimamisha mechi rasmi baada ya wachezaji kushindwa kucheza katika hali hiyo.
Wachezaji wa Yanga walirudi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakisubiri maelekezo zaidi. Baada ya dakika 10, mvua ilianza kupungua na baadhi ya wachezaji wa Yanga walitoka nje kwa ajili ya kuwasalimia mashabiki wao.

Mchezo huo ulikuwa sehemu ya maandalizi ya timu zote mbili kufuatua kusimama kwa ligi. Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi, alikuwa amepanga kutumia mechi hii kujaribu baadhi ya mifumo ya uchezaji na kuwapa nafasi wachezaji wake kupata mazoezi ya ushindani.
Kwa upande wa Singida Black Stars, mchezo huu ulikuwa fursa ya kuonyesha uwezo wao dhidi ya moja ya timu bora zaidi nchini. Licha ya mechi kutomalizika, walionyesha uimara wao katika safu ya ulinzi na nidhamu ya mchezo.

Vikosi vya Mechi:
Singida Black Stars: Metacha (Kipa), Mkumbo, Malonga, Assinki (Nahodha), Trabi, Damaro, Keyekeh, Pokou, Adebayor, Bada, Sowah.
Yanga SC: Khomeiny (Kipa), Kibwana, Kibabage, Andabwile, Boka, Mkude, Maxi, Sureboy (Nahodha), Pacome, Ikangalombo, Sheikhan