Lindi. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Lindi, umesitisha matumizi ya barabara ya Somanga-Mtama kwa muda baada ya mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha wilayani Kilwa, mkoani hapa.
Akizungumzia hilo leo Jumapili Aprili 6, 2025, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Lindi, Emil Zengo amesema wamelazimika kuifunga baada ya maji kujaa kiasi cha barabara kushinda kupitika.

“Kwa sasa tumeshamjulisha Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta, ametoa maelekezo kuhusu usalama wa watumiaji, jambo ambalo ni muhimu,” amesema.
Zengo amesema Besta ameelekeza barabara hiyo ifungwe ili kutoa nafasi ya kuchunguza hali ya uharibifu na kuhakikisha usalama wa watumiaji.
“Tunawashauri wananchi kuendelea kufuatilia taarifa zaidi kutoka mitandao ya kijamii ya Tanroads,” amesema.
Amesema vifaa vya kazi vipo kwenye eneo la tukio na makandarasi wanaendelea na utekelezaji wa majukumu yao ili kurekebisha hali hiyo haraka.

“Maji yatakapopungua tutaanza kufanya kazi ya kurejesha mawasiliano na barabara itafunguliwa mara moja,” amesema.
Zengo amesisitiza usalama wa watumiaji wa barabara ni kipaumbele ndiyo maana imefungwa.
Amesema wananchi wataendelea kupewa taarifa rasmi ya kila hatua inayochukuliwa.