Mabao 30 yamefungwa katika mechi tisa za Ligi ya Mabingwa Ulaya jana usiku huku kukiwa na matokeo tofauti kwa baadhi ya vigogo vya soka barani humo.
Idadi hiyo ya mabao 30 yaliyowekwa kimiani jana imefanya kila mechi iwe na wastani wa mabao 3.2 huku timu nyingi zilizokuwa nyumbani zikitamba kwa kupata ushindi.
Matokeo ya kushangaza zaidi yalikuwa ni kichapo cha mabao 3-1 ambacho Real Madrid ilikipata nyumbani katika Uwanja wa Santiago Bernabeu kutoka kwa AC Milan ambacho kimefanya mabingwa hao watetezi kujikuta wakiwa nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi sita.

Mabao ya Malick Thiaw, Alvaro Morata na Tijjani Reijnders yaliifanya Real Madrid kupokea kipigo cha pili mfululizo nyumbani baada ya kile cha mabao 4-0 ambacho walipewa na Barcelona katika Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’, Oktoba 26 huku kikiendeleza udhaifu wa mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kuruhusu nyavu zao kutikiswa katika siku za hivi karibuni.
Katika Uwanja wa Anfield, wenyeji Liverpool waliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Bayer Leverkusen ambayo yalipachikwa na Luis Diaz aliyefumania nyavu mara tatu na lingine moja likipachikwa na Cody Gapko.
Nchini Uholanzi, PSV Eindhoven ilitumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Philips Stadion kuichapa Girona kwa mabao 4-0 ambayo yalifungwa na Ryan Flamingo, Malik TillmanJohan Bakayoko na lingine moja la kujifunga la Ladislav Krejci na katika mchezo mwingine, Dinamo Zagreb ilipata ushindi wa mabao 4-1 ugenini dhidi ya Slovan Bratislava yaliyofungwa na Dario Spikic, Sandro Kulenovic aliyepachika mawili na lingine moja la Petar Sucic huku lile la wenyeji likipachikwa na David Strelec.
Bao la Thilo Kehrer liliipa ushindi wa bao 1-0 Monaco ugenini dhidi ya Bologna na Celtic iliichapa RB Leipzig kwa mabao 3-1, mabao ya ushindi yakifungwa na Nicolas Kuhn aliyepachika mawili na lingine moja likiwekwa kimiani na Reo Hatate huku la Leipzig likipachikwa na Christoph Baumgartner.
Donyell Malen alifunga bao pekee la ushindi wa Dortmund dhidi ya Sturm Graz, Lille ilitoka sare ya bao 1-1 nyumbani mbele ya Juventus. Bao la Lille lilipachikwa na Jonathan David na lile la Juventus lilifungwa na Dusan Vlahovic.
Sporting Lisbon iliiteketeza Manchester City baada ya kuichapa kwa mabao 4-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Jose Alvalade jijini Lisbon.

Aliyeongoza mauaji ya Manchester City jana ni Viktor Gyokeres ambaye alifunga mabao matatu huku lingine moja likiwekwa kimiani na Maximiliano Araujo na bao pekee la kufutia machozi la Manchester City likifungwa na Phil Foden.