Muziki wa dandi unaelekea wapi? 

Dar es Salaam, Katika mazungumzo ambayo hujitokeza na kupotea katika ulimwengu wa muziki ni dhana kuwa muziki wa dansi Tanzania unapotea. 

Kuna wapenzi wa muziki huo wanaosema hivyo, kuna wanamuziki wanaounga mkono kauli hiyo lakini pia kuna wapenzi wa muziki  na wanamuziki wengine wanaoipinga kauli hiyo.

Kuna wanamuziki wanaodai kuwa muziki wa dansi unashushwa makusudi na vyombo vya utangazaji kwa kutokupiga muziki huo katika vyombo vyao, kuna wapenzi wa muziki wanaodai kuwa muziki wa dansi umeshuka kwa kuwa wanamuziki hawataki kwenda na wakati, kimsingi kuna sura nyingi kuhusu muelekeo wa muziki wa dansi wa Tanzania.

Utofauti huo wa maoni unatokana na mitazamo mbalimbali kuhusu muziki huu, wako wapenzi wa muziki ambao walikuweko wakati muziki wa dansi ulitawala anga za muziki Afrika nzima, wakati wanamuziki wa kila nchi walijitahidi kuwa na aina yao ya muziki. 

Wako pia wanamuziki waliokuweko enzi hizo, nao walijitahidi  kutunga na kupiga muziki uliotokana na mawazo yao halisi na kufanikiwa kuwa na muziki uliotambulika kuwa ni wa Kitanzania. 

Wako wapenzi wa muziki ambao wamezaliwa na kukuta muziki wa dansi ukiwa ni kivuli cha chochote kinachoanzishwa  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na pia kati yao wamepatikana wanamuziki wenye mtizamo huo, hivyo kundi hili linaamini kabisa tatizo la kupotea kwa muziki wa dansi ni kutokana na muziki wa dansi kutoiga kwa ufasaha muziki kutoka Kongo.

Kwa kweli picha ni kubwa zaidi na inahusisha vyombo vya utangazaji, wanamuziki, waandaaji wa muziki, serikali, wafanyabiashara wenye kutumia muziki kama  vile wamiliki wa vyombo vya muziki, wamiliki wa baa na kumbi za starehe, wasambazaji wa muziki, mapromota, mameneja na kadhalika kwani hawa wote kwa namna moja au nyingine wanahusika  katika kuufikisha muziki wa dansi ulipo. 

Nianze na vyombo vya utangazaji, hakika kuna ukweli mkubwa kuwa muziki wa dansi umefika ulipo kutokana na mchango wa vyombo vya utangazaji. 
Mwanzoni mwa miaka ya 90 mara baada ya vyombo huru vya utangazaji  kuanza, wanamuziki wa muziki wa dansi wakajikuta vituo vya radio vinaongezeka lakini  kazi zao zikaanza kukosa nafasi ya kupigwa katika  vituo hivyo.

Sababu kubwa ya nyimbo zao kutopigwa katika vituo hivyo  ilielezwa kuwa kazi hazikuhifadhiwa  katika ubora stahiki, wanamuziki walianza kudaiwa kuhifadhi ‘master’ zao zikiwa katika kanda aina ya Chrome, muda mfupi baada ya hapo vituo vilivyokuwepo vikawa vinapokea nyimbo zilizohifadhiwa katika kanda zilizokuwa katika mfumo wa ‘mini disc’.

Kulikuwa na studio chache mno ambazo ziliweza kutoa muziki na kuweka katika Chromena mini disc, bendi zikaanza kupotea katika vyombo vya utangazaji. 

Ni katika kipindi hiki muziki kutoka nchi jirani ya Kongo ukaanza kupata umaarufu mkubwa sana katika redio hizo mpya,  bendi za Kikongo nyingi zikaanza kupata mialiko mingi nchini na awamu mpya ya utwala wa muziki wa Kikongo nchini ukarudi tena.

Awamu ya kwanza ilikuwa katikati ya miaka ya 60 wakati bendi za hapa nchini zilikuwa zinashindana kunakili kazi zilizorekodiwa na bendi za kutoka Kongo, katika kipindi hicho serikali iliwaita wanamuziki na kuwataka waache kuiba nyimbo za Kikongo, jambo hilo lilifufua ubunifu uliokuwepo kuanzia  miaka na bendi nyingi ambazo nyimbo zao ni maarufu mpaka leo zilirekodiwa katika kipindi hiki. 

Ili kupata nafasi katika soko la muziki, bendi za muziki wa dansi zikaanza kuiga kila kinachotoka, tofauti ikawa ni lugha tu na hakika ndiyo hali ilivyo mpaka leo.

Wanamuziki nao wana mchango mkubwa katika kufikisha muziki ulipo. Asilimia kubwa ya bendi siku hizi hazifanyi mazoezi hivyo basi hazirekodi kabisa  nyimbo mpya.

Bendi nyingi zinategemea nyimbo zilizorekodiwa na bendi miaka ya 90 na kurudi nyuma, na hata nyimbo hizo kwa vile hazifanyiwi mazoezi kabla ya kupigwa hadharani huwa hazina utamu ule wa nyimbo halisi.

Kimsingi bendi karibu zote hazifuati utawala bora wa uendeshaji wa bendi. Kundi la wamiliki wa vyombo vya muziki, wamiliki wa baa na kumbi za starehe nalo haliwezi kuachwa katika kubeba lawama ya kuufikisha muziki ulipo.

Kuna bendi ambazo mmiliki wa vyombo anatoa amri ya aina ya muziki ambao upigwe, na mara nyingi wanamuziki huamriwa kupiga muziki wa ‘kisasa’, maana yake ikiwa ni muziki wa sebeni.

Wamiliki wa baa hulazimisha muziki kupigwa kwa kelele ili kuita wateja, hivyo wateja waliomo kwenye bar hujikuta wakipigiwa kelele  badala ya muziki.

Kwa vile jambo hili limeendelea muda mrefu, hata wanamuziki nao wanaona kupiga muziki kwa kelele ndiyo kuonesha ufanisi katika muziki, haya yote yanachangia sana kuonesha kuwa muzki wa dansi umeshuka. 

Bendi zirudi kwenye nidhamu za uendeshaji wa muziki za zamani na pia kuanza kutumia ubunifu badala ya kuwa mafundi wa kunakili tungo za wanamuziki wengine.