
Dar es Salaam. Muziki na filamu ni ndugu, japokuwa muziki ulikuweko kabla ya filamu. Filamu za kwanza zilipoanza kutengenezwa, kulikuwa hakujagundulika utaalamu wa kuunganisha picha na sauti, hivyo sinema hizo za kimya kimya za awali za kati ya mwaka 1895 hadi 1927zilijulikana kama kama ‘silent films’.
Filamu zilitumia mabango yaliyoandikwa maneno kuonyesha nini muigizaji alikuwa akisema, wanamuziki walikodishwa kupiga muziki laini wakati filamu inaonyeshwa, baadaye kukawa kunatumika gramophone, chombo ambacho ni cha kupiga santuri za muziki wakati filamu inaonyeshwa.
Filamu za kwanza kuunganishwa filamu na sauti zilianza mwaka 1930 na ziliitwa ‘talkies’ au ‘talking pictures’. Teknolojia hiyo ikafungua uwanda mpana wa matumizi ya muziki katika filamu.
Muziki ukaendelea kutiliwa umuhimu mkubwa katika utengenezaji wa filamu bora, na katika filamu zote kukawa na msisitizo maalumu kuhusu aina ya muziki utakaosindikiza filamu.
Muziki hufanya kazi muhimu sana katika filamu, husaidia kuongeza hisia ya tukio, husaidia kuhadithia tukio, na kadri muziki ulivyo bora ndivyo na utamu wa filamu unavyozidi.
Uhusiano huu wa muziki na filamu uliendelea kukua kiasi cha kuweza kusaidia hata kukua kwa tasnia hizi mbili.
Filamu zikaweza kupata umaarufu kutokana na muziki mzuri au muziki ukaweza kupata umaarufu kutokana na ubora wa filamu. Kuna mifano mingi ya jambo. Waliokuwa wapenzi wa filamu za ‘cowboys’ waliweza kuwaigizaji wapiga magitaa kama Roy Rodgers, na Gene Autry wakipata umaarufu pia kama wanamuziki na nyimbo zao zilizotumika kwenye filamu kuuzwa sana.
Katika filamu za kihindi uhusiano wa muziki na filamu ni mkubwa sana, watu wengi wanazifahamu nyimbo kama Kuch kuch hota hai, iliyokuwemo katika filamu Kuch Kuch hota hai , nyimbo mbili zilizoitwa Kabhi kabhi Mere Dil Mein zilizokuwa katika filamu iliyoitwa Khabi Khabi, Goro ki na Kalo ki, Jimmy, na wimbo Disco Dancer zilizokuwa katika filamu iliyoitwa Disco Dancer ni mifano ya nyimbo zilizokuwa na katika filamu mbalimbali za Kihindi.
Nyimbo hizi zimefanya filamu zipendwe zaidi, na hakika filamu zimewezesha nyimbo hizi kupendwa na kuingiza fedha nyingi pia.
Wahindi walijenga utamaduni wa kutengeneza filamu nzuri za utamaduni wao, ambazo ziliambatana na muziki ulitungwa na kupigwa na kuimbwa na kati ya mahadhi ya kwao kwa kuwatumia wanamuziki bora waliowahi kutokea India, waimbaji wa kike kama Lata Mangeshka na dada yake Asha Bhosle, waimbaji maarufu wa kiume akina Mukesh, Mohammed Rafi na wengineo waliweza kurekodi maelfu ya nyimbo ambazo waigizaji walizitumia na kuonekana wanaimba katika filamu zao na kupata umaarufu duniani kote.
Watu wengi ambao hawakujua hata maana ya neno moja la Kihindi walijikuta kuwa mashabiki wakubwa wa filamu za Kihindi, muziki ukiwa sababu mojawapo.
Lakini hebu tuangalie hali ya uhusiano kati ya tasnia ya filamu na muziki hapa kwetu. Pamoja na kuwa tasnia hizi bado ziko chini sana katika ramani ya filamu na muziki ulimwenguni, hakuonekani mpango wowote wa kuunganisha nguvu ili kupata faida ya pamoja.
Katika kipindi cha karibuni watu muhimu katika tasnia ya filamu wamekuwa wakionyesha waziwazi kuwa tasnia hiyo ni muhimu kuliko tasnia ya muziki na hakika kudai ni muhimu kuliko tasnia nyingine za sanaa.
Filamu na muziki zina mambo mengi ambayo ni ya pamoja. Sheria za hakimiliki zinazoongoza muziki ni zilezile zinazoongoza filamu, matatizo ambayo sekta ya filamu inayapata sasa ni yale yale ambayo sekta ya muziki imeyapitia.
Biashara ya kuuzwa kwa kazi haramu za ndani na za nje ndizo zimeua biashara ya kuuza kazi za muziki na vivyo hivyo biashara ya kuuza filamu. Ningeshauri sana kwamba tasnia hizi mbili ziangalie na zijifunze kutoka India kwa hili.
Nchi hiyo imejenga tasnia za muziki na filamu kwa misingi ya utamaduni wa nchi yao. Na kwa kutumia raslimali hii muziki na filamu kutoka nchi hii zimekuwa za kipekee na kuweza kusambaa dunia nzima.
Wasanii wenye hofu na ubora wa utamaduni wao huona utamaduni wa nchi nyingine ni bora na kuamua kuuiga kwa nguvu zote na kwa daima hubakia kuwa kivuli cha wenye utamaduni ule.
Filamu na muziki wetu ni mfano mkubwa wa uoga huu, wa kudhania tusipofanya kama wengine tutakosa ‘soko la kimataifa’, kazi zetu za sanaa zinaiga tungo, maudhui, na hata vitu vya kawaida kama mavazi, kuiga sio dawa ya kupata kazi bora bali ni njia ya kutengenza soko kwa unaowaiga.
Swala la kupata faida kutokana na kazi za filamu na muziki hakika ni jambo muhimu sana, lakini biashara isiruhusiwe kuondoa Utanzania wetu.
Hapa sasa ni nafasi ya serikali, nchi zote ambazo zina maendeleo katika kazi zake za sanaa zimeweka kanuni za kulinda sanaa za ndani. Kanuni hizi hupanga pia kiasi cha kazi za nje kitakachotumika katika vyombo vya utangazaji kama TV na redio, kwani vyombo hivi ni muhimu sana katika kujenga tabia za wananchi.
Ni muhimu sasa kulazimisha kipengele hiki ili kubadili mwelekeo wa kizazi kipya na kijacho cha Watanzania.