Arusha. Sakata la mkazi wa Daraja Mbili, jijini Arusha Neema Kilugala aliyedai kubadilishiwa mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, limechukua sura mpya baada ya Wizara ya Afya kumsimamisha kazi muuguzi aliyemhudumia mzazi huyo ili kupisha uchunguzi.
Muuguzi huyo alidai kuchanganya vitenge na vya mtoto mwingine hivyo akaahidi kwenda kubadilisha ambapo licha ya kufanya hivyo hali ya sintofahamu iliendelea.
Kufuatia hali hiyo Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Katibu Tawala wa Mkoa pamoja na Jeshi la Polisi Arusha, limechukua hatua nyingine ikiwemo kuchukua sampuli za wazazi waliojifungua kipindi hicho na za watoto kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA), kwenda Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Neema alijifungua kwa njia ya upasuaji Machi 24, 2025 na kudai baada ya kujifungua alioneshwa mtoto wake wa kike na muuguzi akiwa mzima, hata hivyo aligundua amebadilishiwa mtoto wake baada ya kuletewa mtoto aliyekuwa amefungwa vitenge ambavyo si vyake.

Mawakili kutoka Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia,wakimsikiliza Neema Kilugala,mkazi wa Daraja Mbili,leo Jumatano Aprili 2,2025,anayedai kubadilishiwa mtoto wake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mt.Meru baada ya kujifungua kwa upasuaji. Picha na Janeth Mushi
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo leo Jumatano Aprili 2, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Roida Andusamile na kueleza kuwa uchunguzi ukikamilika taarifa rasmi zitatolewa na hatua stahiki zitachukuliwa.
“Kufuatia hali hiyo Wizara ya Afya kwa kushirikiana na ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha pamoja na Jeshi la Polisi limechukua hatua ya kuchukua sampuli za wazazi waliojifungua kipindi hicho pamoja na za watoto kwa ajili ya uchunguzi wa DNA,”
“Pia imemsimamisha kazi muuguzi aliyemhudumia ili kupisha uchunguzi. Baada ya uchunguzi kukamilika taarifa rasmi zitatolewa na hatua stahiki zitachukuliwa,” imeongeza taarifa hiyo
Akizungumza na familia hiyo nyumbani hapo Wakili Maleko aliwaeleza kuwa wamefika hapo kwa ajili ya kuwasikiliza na kukusanya nyaraka muhimu kisha kuongozana nao hadi hospitalini hapo ili wasikilize upande huo wa pili, kisha wajue mahali pa kuanzia kwa ajili ya kuwasaidia kupatia msaada wa kisheria.
“Tukiwa katika utekelezaji wa kampeni hii tulipata malalamiko ya Neema na mama tumeenda kumtembelea na kusikia kutoka kwa upande wake namna ilivyokuwa na mama yake ambaye alikuwa karibu yake, tumekuja kusikiliza na upande wa uongozi wa hospitali,”

“Nao wametueleza na sasa inasubiriwa majibu ya vinasaba na Polisi imeshafanya upande wake, majibu kwa vyovyote ambavyo itakuwa hatua za kisheria zitafuata mkondo wake ikiwemo mtumishi aliyefanya hivyo ambaye kwa sasa yuko katika mikono ya sheria,” amesema
“Mtoto ambaye Neema alipewa ambaye hamtambui ni kweli mtoto huyo amefariki na daktari ametueleza alikuwa na changamoto za upumuaji tangu azaliwe, tumemuuliza amesema mtoto huyo wamemhifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti hapa, wakisubiri haya yanayoendelea,” ameongeza
Msingi wa malalamiko
“Ninachotaka ni mtoto wangu, Wamenichukulia mtoto wangu pale Mount Meru ninachotaka tu wanirudishie mtoto wangu mweupe mwenye alama mkononi, naombeni jamani mnisaidie nimpate mtoto wangu”.
Ni maneno yenye uchungu yaliyoambatana na machozi ya kilio na kwikwi yanayomtoka Neema, akizungumza na waandishi wa habari, Neema amesema kuwa Alhamisi Machi 20,2025 alipata changamoto ya kuanguka baada ya kukumbwa na kizunguzungu huku akihisi maumivu makali sehemu za mgongo.
Alipelekwa Mount Meru saa tano asubuhi na kukata faili kisha kuelekezwa aelekee chumba cha kujifungulia kwa ajili ya uchunguzi wa madaktari wa eneo hilo.
“Baada ya vipimo daktari alisema natakiwa nifanyiwe upasuaji siku ya Ijumaa hivyo nielekee wodi ya mapumziko kwa ajili ya maandalizi hayo siku inayofuata,” amesema Neema.
Neema anasema kuwa baada ya kufika katika chumba cha mapumziko nesi wa zamu alisema hayuko kwenye orodha hivyo asubiri hadi apangwe kama hakutatokea dharura yoyote.
“Siku ya Ijumaa asubuhi nikaambiwa natakiwa vifaa ili nifanyiwe upasuaji wa kujifungua hivyo nilimpigia simu mama yangu akaleta vifaa na nikafanyiwa maandalizi yote hadi kupelekwa chumba cha upasuaji kabla ya muda kidogo kutolewa na kuambiwa nitafanyiwa jioni lakini pia ikakwama,”
“Wakasema nisubiri hadi Jumamosi asubuhi lakini pia sijafanyiwa nikaambiwa nisubiri hadi Jumatatu ndio nifanyiwe hata hivyo sikukata tamaa nilisubiri hadi Jumatatu kweli nikafanyiwa upasuaji asubuhi saa nne”.
Neema anaeleza kuwa baada ya kufanyiwa upasuaji alifanikiwa kumuona mtoto wake na muuguzi kumjulisha kuwa mtoto ni mzima na yuko vizuri mwenye afya njema akiwa na uzito wa kilo 3.1.
“Baada ya kuambiwa hivyo na kumuona nilimshukuru Mungu na wakanipeleka chumba cha kupumzika, kabla ya majira ya saa saba kuletewa mtoto huku amefungwa vitenge ambavyo si vya kwangu”
“Nilishangaa sana nikamwambia mama mbona huyu mtoto ana vitenge si vya kwangu? Ndio mama naye kuangalia na kwenda kumwita nesi aliyemleta mtoto akaja kumchukua”
Neema anasema kuwa baada ya nesi kumchukua mtoto yule huo ndio ukawa mwisho wa kumuona mtoto hadi kupewa taarifa za kifo cha mtoto wake.
“Sijui kilichotokea huko maana walirudi bila mtoto huku nikiambiwa amehifadhiwa chumba cha joto nikauliza chumba cha joto vipi wakati mtoto wangu hakuwa na shida yoyote ndio wakaendelea kunizungusha kuwa watanipa kesho yake niache apumzike ila yupo vizuri,’
“Asubuhi naitwa kwenda kumuona mtoto nashangaa naonyeshwa mtoto ambae sio yule mtoto wangu, kwa sababu tumemkuta anaumwa na nimeambiwa ana shida ya moyo kuwa mkubwa”
“Mtoto wangu wamemchukua na kwa vile tu nilifanyiwa operesheni kwa sababu wasingemchukua mtoto wangu, Mimi namtaka tu mtoto wangu mwenye kilo 3.1 na mweupe tena alama mikononi kama yangu, si huyu mweusi mwenye kilo 2.285 tena ana matatizo ya moyo kuwa mkubwa” amesema Neema.
Naye Sabina Andrea (mama wa Neema) amesema kuwa wamempeleka mtoto wake Hospitali Alhamisi baada ya kupata changamoto ya kizunguzungu kabla ya kutakiwa kupeleka vifaa kwa ajili ya kujifungua.
Amesema kuwa baada ya kuleta vifaa ili mwanae afanyiwe upasuaji wa kujifungua, bado hakufanyiwa Ijumaa hiyo hadi Jumatatu ndio wakamfanyia kabla ya kugundua kuwa wamebadilishiwa mtoto.
“Niliitwa mchana kwenda kumuona mtoto lakini nilipoingia ndio mwanangu ananiambia mbona nguo si za mtoto ndipo nikatoka kwenda kumuita nesi na akaja kumchukua mtoto akabadilishe nguo lakini wakati namfuata akakimbia na kupita mlango wa nyuma”
“Nimefika huko kumkuta nesi namuuliza mtoto anasema amemrudisha chumba cha joto na kunionyesha mtoto aliye na mipira puani tena akiwa njiti tofauti na yule aliyemleta mwanzo ndio mzozo ukaanzia hapo kabla hatujafukuzwa hospitalini” amesema mama huyo.
Mama huyo ameiomba Serikali kumsaidia haki ya mtoto wake ipatikane ili waweze kupata mtoto wao ikiwemo vipimo vya DNA kufanywa kwa watoto wote waliozaliwa siku hiyo.
“Mimi hili jambo limeniathiri kisaikolojia kwani nina watoto sita na kati ya hao watano nimejifungulia pale nina wasiwasi hata hao nilionao labda kuna niliyebadilishiwa maana kuna mmoja baba yake ameniambia siyo mtoto wake,” ameongeza