
Mlimba. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ametoa agizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dastan Kyobya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Jamal Idrisa kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kumpongeza Gordian Maganga (28), Ofisa Muuguzi Daraja la Pili wa Zahanati ya Ikwambi, kwa kazi kubwa na ya kujitolea anayofanya.
Maganga amepongezwa kwa moyo wa kujituma na kujitolea kuvuka mito na kupitia mazingira magumu ili kuwafikia wananchi walioko katika vijiji vya mbali kwa ajili ya kutoa chanjo kwa watoto.
Malima amesema Maganga ni mfano wa kuigwa na unapaswa kutambuliwa rasmi ili kuhamasisha watumishi wengine kuwa na moyo wa uzalendo na utumishi uliotukuka kwa jamii.
Agizo hilo amelitoa leo Alhamisi Mei Mosi, 2025 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, iliyofanyia kimkoa katika Uwanja wa Jamhuri, Manispaa ya Morogoro.
Malima amesema Maganga anastahili pongezi na motisha ili kuwahamasisha wauguzi na watumishi wengine wanaofanya kazi katika mazingira yenye changamoto nyingi.
“Mimi nimeona picha ya muuguzi huyo jana, nilionyeshwa na mtu mmoja. Kiukweli, inaonyesha namna alivyojitoa kuvuka mto wenye maji mengi akiwa amebeba sanduku la chanjo kwenda kuwachanja watoto kwenye kijiji cha pili. Huu ni moyo wa kipekee wa uzalendo, amekubali kujitosa kwenye maji kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto wetu,” amesema Malima.
Ameongeza kuwa kutokana na ujasiri huo wa kipekee, alitegemea kuona yupo kwenye maadhimisho hayo ili apatiwe heshima ya kupongezwa mbele ya hadhira.
“Lakini kwa kuwa hayupo, viongozi wa wilaya mnapaswa kuandaa utaratibu maalumu wa kumtia moyo kwa kumpongeza,” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa pia ameahidi kumpatia Maganga zawadi ya Sh1 milioni kutoka ofisi yake akamuelekeza Mkuu wa Wilaya kufuatilia malipo hayo kupitia Katibu Tawala wa Mkoa ili fedha hizo zimfikie mtumishi huyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya Kyobya naye amempongeza Maganga kwa kujitolea kwa moyo mkubwa kuhakikisha watoto wanapata chanjo, bila kujali hali ya hewa wala changamoto ya kuvuka mto mkubwa.
“Hii ni wiki ya kampeni ya kitaifa ya chanjo. Muuguzi huyu alibeba sanduku la chanjo kutoka kituo chake cha kazi hadi kijiji cha Miyomboni, akipambana na mvua kubwa na kuvuka mto uliojaa maji kuhakikisha watoto wanapata huduma. Ni vijana wachache sana waliobaki na moyo kama huu,” amesema Kyobya.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Maganga amesema aliamua kuvuka mto huo kwa lengo la kuwafikia watoto waliokuwa wanakosa chanjo kutokana na ugumu wa kuwafikisha kliniki, hasa kipindi hiki cha mvua.
Amesema baadhi ya wazazi huenda shambani na wengine hushindwa kuuvuka mto huo.
Maganga amesema huo siyo mto wa kwanza kuuvuka, amekuwa akivuka mara kwa mara kwenda kutoa huduma za afya Kijiji cha Miyomboni.
Hata hivyo amesema Aprili 29, 2025 mto huo ulijaa maji mengi hali ilimpa wakati mgumu tangu aanze kazi katika zahanati hiyo.
“Tangu niajiriwe miezi minne iliyopita katika Zahanati ya Ikwambi, nimekumbana na changamoto nyingi ikiwemo ya miundombinu duni ya barabara. Hata hivyo, sikukata tamaa, nimejifunza kuvumilia kwa sababu naipenda kazi yangu na natambua umuhimu wa huduma ninayotoa kwa watoto hawa, ndiyo kizazi cha kesho,” amesema Maganga.
Amesema yeye si mzaliwa wa Morogoro, anatoka Kigoma, baada ya kuhitimu chuo mwaka 2023, alifanya kazi ya kujitolea kwa miezi minane katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora kabla ya kupata ajira ya kudumu.
Amesema hana uzoefu wa maisha ya kuvuka mito, lakini alipofika kituoni hapo alilazimika kujifunza ili aweze kuwafikia wananchi, hasa watoto.
“Changamoto kama hizi ni za muda mfupi, lakini kazi ni ya kudumu. Siwezi kuacha kazi kwa sababu ya mazingira. Hii ndiyo taaluma yangu, na kupata ajira si jambo rahisi kwa vijana wengi wa sasa,” amesisitiza.
Amewashauri vijana wengine waliopata ajira kuwa wavumilivu na kuthamini nafasi walizopata badala ya kukimbia vituo vya kazi au kutafuta visingizio vya uhamisho, kwa sababu kufanya hivyo kunawanyima wananchi huduma muhimu.