Muqawama wa Palestina: Republican au Democratic; Serikali zote za Marekani zinaiunga mkono Israel

Kamati ya makundi ya mapambano na Muqawama ya Palestina imetoa taarifa kuhusu ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani na kutangaza kuwa, hakuna tofauti baina ya Warepublican na Wademokrat; Kwa sababu serikali zote za Marekani zimekuwa waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wa Israel na washirika wake katika mauaji dhidi ya taifa la Palestina.

Idara ya Habari ya Kamati za makundi ya Mapambano ya Palestina imeeleza kuwa, vyama vya Republican na Democratic ni nyuso mbili zinazofanana katika kuendeleza dhulma ya Marekani na uungaji mkono kwa Uzayuni katika vita vya mauaji ya kimbari yanayofanyika dhidi ya watu wa Palestina, Lebanon na Umma mzima wa Kiislamu.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa: Marekani ni nembo ya dhulma na ubeberu, na inaiburuta dunia kwa mkono wa chuma na moto, na imewasha moto wa chuki duniani kote.

Taarifa ya Kamati za makundi ya Mapambano ya Palestina imesisitiza kuwa: “Marekani inaua taifa letu la Palestina na Lebanon kwa kutumia taasisi, vyama, mabunge, makombora yake, mabomu na silaha za uharibifu, lakini licha ya hayo yote, Muqawama wa Lebanon na Palestina utaibuka na ushindi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.”