Muqawama wa Kiislamu wa Iraq washambulia ngome na vituo vya utawala wa Kizayuni

Muqawama wa Kiislamu wa Iraq umetangaza kuwa umefanya shambulizi la ndege isiyo na rubani kwenye kituo cha kijeshi kusini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina bandia la Israel.

Kwa mujibu wa shirika la habari la  IRNA, Muqawama wa Kiislamu wa Iraq umetoa taarifa leo na kutangaza kuwa umefanya shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye kituo cha kijeshi kusini mwa maeneo hayo yanayokaliwa kwa mabavu, sambamba na kusisitiza kuwa, kuponda  ponda vituo vya kijeshi na ngome za adui Mzayuni kunaendelea kwa sura ya kuongezeka siku hadi siku.

Jana Jumatatu Muqawama wa Kiislamu wa Iraq ulifanya oparesheni sita dhidi ya ngome na  vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni.

Katika miezi michache iliyopita,  Muqawama wa Kiislamu wa Iraq umevishambulia vituo nyeti na muhimu katika maeneo tofauti ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel,  ikiwa ni pamoja na bandari ya Eilat, Golan na Bonde la Jordan.

Muqawama wa Kiislamu wa Iraq unaichukulia Marekani kuwa mhusika mkuu wa mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na  utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza na umesisitiza kuwa, utaendeleza oparesheni zake dhidi ya vituo vya kijeshi vya  utawala huo haramu madamu mashambulizi ya jeshi la Israel dhidi ya Ukanda wa  Gaza na Lebanon yangali yanaendelea.