Muqawama wa Kiislamu wa Iraq waendeleza mashambulizi dhidi ya vituo vya wanajeshi wa Kizayuni

Muqawama wa Kiislamu wa Iraq umetangaza kuwa umekilenga kituo muhimu katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina (Israel).

Muqawama  wa Kiislamu wa Iraq umetangaza katika taarifa yake uliyotoa leo kuwa, Mujahidina wa Muqawama wa Kiislamu wa Iraq wameshambulia kituo muhimu cha utawala wa Kizayuni katikati mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kwa kutumia ndege isiyo na rubani ili kukabiliana utawala huo ghasibu, kuunga mkono mataifa ya Palestina na Lebanon na kutoa jibuu kwa mauaji ya raia wakiwemo watoto, wanawake na wazee.

Ijumaa ya jana,  wanamuqawama  wa Kiislamu wa  Iraq walifanya oparesheni sita pia za ndege zisizo na rubani dhidi ya vituo kadhaa kaskazini, katikati na kusini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Katika wiki na miezi iliyopita, Muqawama wa Iraq ulivilenga vituo nyeti na muhimu vilivyoko Eilat, kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Katika shambulio muhimu zaidi la ndege isiyo na rubani lililofanywa na Muqawama wa Kiislamu wa Iraq katika kambi ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni katika eneo la Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu, askari 25 wa utawala huo waliuawa na kujeruhiwa.
Muqawama wa Kiislamu wa Iraq umetahadharisha kuwa, iwapo utawala wa Kizayuni utaendelea na mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza, basi utazidisha oparesheni zake dhidi ya ngome za kijeshi za utawala huo ghasibu.