
Windhoek. Ijumaa iliyopita, Rais mteule wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah aliapishwa kuwa Rais wa tano wa Namibia baada ya kushinda uchaguzi wa Novemba 27, 2024 akiwa ni mgombea wa chama tawala cha Swapo.
Nandi-Ndaitwah siyo jina geni kwenye siasa za Namibia, wengi wanamfahamu alivyoshiriki harakati za ukombozi wa taifa hilo hadi lilipopata uhuru mwaka 1990 na yeye kushiriki katika serikali ya kizalendo iliyoundwa.
Hata hivyo, upande wa pili wa maisha yake ya familia haujulikani na wengi. Mume wake, Epaphras Ndaitwah, ambaye ni Luteni Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Namibia, anasimulia namna alivyokutana na mke wake wakiwa uhamishoni.
Anasema anakumbuka alivyokutana Netumbo katika uwanja wa ndege wa Zambia mwaka 1979.
“Nilipigwa na butwaa! Alikuwa mdogo na anaiwakilisha nchi yake katika ardhi ya kigeni,” anasema Epaphras.
Anasema huyo alikuwa Ndemupelila Netumbo Nandi, mwanaharakati mdogo kutoka Namibia ambaye alifanya kazi Lusaka katika idara ya diplomasia na siasa ya chama cha Swapo.
Mwaka 1983, akiwa Tanzania, alimuoa Netumbo, ambaye wakati huo alikuwa kiongozi anayetengenezwa.
Wakati Epaphras alipokuwa akihudumu katika nafasi za juu za kijeshi kama Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Namibia, hadi alipostaafu mwaka 2013, mke wake aliendelea kupanda ngazi kisiasa.
Epaphras anasema kuwa haitakuwa haki kwake kuzungumzia uwezekano wa mkewe kuwa Rais. “Hii itakuwa na upendeleo,” anasema.
“Kwa kuangalia nafasi zote alizohudumu, unaweza kuona majukumu na wajibu huo ulikuwa ukijijenga hadi sasa,” anasema.
“Nyumbani, yeye ni mke wangu, na mimi ni mume wake. Anaweza kupika. Hapendi niache chakula alichopika,” anasema.
Wanandoa hao wana watoto watatu na wajukuu wanne. Mtoto wa pili wa Nandi-Ndaitwah ni Ndelitungapo Ndaitwah, wakili aliyeifanya kazi katika kampuni ya Sisa Namandje na Co. hadi mwaka jana.
Anasema mara chache humuona mama yake akipumzika.
“Kadiri ninavyokua ninagundua kuwa yeye kila wakati anafanya kazi, kwa sababu anapenda sana kile anachofanya,” anasema Ndelitungapo.
Anasema Nandi-Ndaitwah “kimya kimya” anafadhili elimu ya watoto wengi.
Ofisa Mkuu wa Uhusiano wa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini humo, Smile Shafuka anasema kuwa uhusiano wake na Nandi-Ndaitwah ni kama wa mama na binti.
“Nje ya ofisi, wakati mwingine namuita kwa jina lake la ukoo, Mkwanangobe. Anakubali kukaa chini na kucheza owela (mchezo wa jadi), na anapenda kula ombidi (spinachi) na oshifima (uji),” anasema.
Epaphras ni nani?
Luteni Jenerali (mstaafu), Epaphras Ndaitwah, aliyezaliwa Desemba 13, 1952, ni mwanadiplomasia wa Namibia, alihudumu kama ofisa wa jeshi na sasa ni mume wa Rais wa Namibia.
Alikuwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Namibia (NDF) kuanzia Januari 24, 2011 hadi Desemba 31, 2013 alipostaafu.
Alizaliwa katika Mkoa wa Ohangwena, alijiunga na tawi la kijeshi la Swapo, Jeshi la Ukombozi la Watu wa Namibia (PLAN), mwaka 1974 na alishiriki katika mapambano ya uhuru wa Namibia akiwa na majukumu mbalimbali.
Alifanya mafunzo ya kijeshi nchini Russia, Yugoslavia, India, Nigeria, Zambia na Tanzania. Katika uhuru wa Namibia mwaka 1990, Epaphras alikuwa msaidizi wa kwanza wa kijeshi kwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi (CDF), Dimo Hamaambo.
Alikuwa na cheo cha Luteni Kanali wakati huo. Alikua Naibu Kamanda wa Jeshi mwaka 1997. Hadi mwaka 2006, alihudumu kama mjumbe wa Namibia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Alipandishwa cheo kuwa jenerali, mwaka 2008 na aliteuliwa kuwa Mkuu wa Operesheni, Mipango na Mafunzo hadi cheo cha Luteni Jenerali mwaka 2011 alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Namibia (CDF), akimrithi Luteni Jenerali Martin Shalli.
Alitumikia nafasi hiyo hadi mwishoni mwa mwaka 2013 wakati Luteni Jenerali, John Sinvula Mutwa alipoteuliwa kuwa CDF mpya.
Mwaka 2007, Ndaitwah alikamilisha shahada ya uzamili katika masomo ya Mikakati kutoka Chuo Kikuu cha Ibadan, Nigeria. Mwaka 2011, alisoma usimamizi wa umma katika chuo cha Polytechnic cha Namibia.
Epaphras alifanya kazi katika Chuo cha Usimamizi cha Kimataifa kwa miaka mitano kama Mhadhiri Mkuu na Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Mikakati na Utawala wa Biashara kabla ya kuwa mshiriki wa Baraza la Utawala kwa miaka minne ambayo jumla yake ilikuwa miaka tisa.
Alijiondoa kutoka IUM Mei 16, 2024. Ameandika vitabu viwili vilivyoitwa “Maisha na Maoni ya Mwanajeshi: Mtazamo wa Mwandishi na Uongozi wa Kimkakati na Usimamizi – Miongozo ya Mwelekeo.
Katika kipindi cha kazi yake, pia, aliandika makala zaidi ya 40 kwenye magazeti ya Namibia na aliandika makala moja iliyochapishwa katika Jarida la Vikosi vya Silaha vya Afrika.