Mukwala aiokoa Simba jiooni Kigoma

Usimkatie mtu tamaa ndio maneno ambayo unaweza kuyatumia kwenye ushindi wa Simba ikiwa ugenini baada ya kuichapa Mashujaa kwa bao 1-0, ushindi ukipatikana sekunde za mwisho.

Simba ilipata bao hilo katika dakika ya saba kati ya sita zilizoongezwa na mwamuzi Omary Mdoe kutoka Tanga baada ya zile tisini kutimia likifungwa na mshambuliaji Steven Mukwala kwa kichwa akimalizia kona ya kiungo wake Awesu Awesu.

Bao lilikuwa nje

Simba ilihaha kupata ushindi katika mchezo huo lakini kumbe mpishi wa bao na hata mfungaji wote waliwasahau nje kufuatia wawili hao Awesu na Mukwala kuanzia nje wakiingia kipindi cha pili na kutengeneza ushindi huo muhimu kwa Wekundu hao.

Ushindi huo wa Simba unakuwa wa saba msimu huu kwenye mechi zao tisa walizocheza ikifikisha pointi 22, ikiishusha Singida Blacka Stars iliyokuwa nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Johola mtata

Kipindi cha kwanza Simba ililazimika kulia na kipa wa Mashujaa Eric Johola ambaye alisimama imara kulilinda lango lake akiokoa mashuti makali  yaliyokuwa yanaelekea wavuni.

Dakika ya 16 kiungo mshambuliaji Kibu Denis wa Simba aliachia shuti kali kupitia mpira wa adhabu ndogo lakini Johola alilipangua kwa umakini.

Kama haitoshi kipa huyo tena alifanya kazi nyingine bora dakika ya 20 akiokoa shuti la Kibu aliyesetiwa vizuri na  Fabrice Ngoma aliyetangulia kukutana na kigugumizi cha miguu kumalizia krosi ya mshambuliaji Leonel Ateba.

Camara bila majaribio

Simba hata kama ingeamua kucheza bila kipa ingewezekana kwenye mchezo huu baada ya Mashujaa kumaliza dakika dakika tisini bila shuti hata moja lilolenga lango.

Tofauti na michezo mingine, mechi hii Simba ilikuwa inapiga mipira mirefu na tofauti na pasi nyingi za nyuma ambazo ilikuwa ikicheza kwenye michezo kadhaa iliyopita.

Mashabiki wachache

Mashujaa haikupoteza pointi tatu peke yake ikapoteza pia mapato ya kutosha baada ya idadi ndogo ya mashabiki walioingia kutazama mchezo huo tofauti na mechiu za nyuma baina ya timu hizo ambazo ziliingiza mashabiki wengi na kuufanya uwanja huo kufuruka.