
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema hawezi kutoa ahadi ya timu yake kufunga idadi kubwa ya mabao katika mechi ya ligi kuu dhidi ya Pamba Jiji kesho Alhamisi, Oktoba 3 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ingawa kipaumbele chake ni kupata ushindi.
Gamondi amesema kuwa jambo la muhimu katika mchezo wa soka ni kupata ushindi pasipo kuangalia idadi ya mabao kwa vile siku hazifanani.
“Siwezi kuahidi zaidi ya kujitolea, kucheza mpira mzuri na kutoa kila tulichonacho kwa ajili ya wananchi. Kufunga mabao ni jambo zuri na kitu kizuri zaidi katika mpira wa miguu ni bao lakini wakati mwingine unaweza usifunge au kufunga bao moja inatosha.
“Mimi kwangu kwa sasa tunacheza ligi, mechi 30. Tumecheza mechi tatu, pointi tisa nikona furaha sana kwa vile lengo la kwanza ni kufunga bao. Kwangu mimi hakuna kitu cha muhimu zaidi ya kushinda mechi,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema anategemea kukutana na kibarua kigumu mbele ya Pamba ambayo bado haijaonja ushindi kwenye Ligi Kuu msimu huu.
“Nimeichambua nikabaini ni timu ambayo imejipanga vyema kwenye ulinzi lakini wanahitaji njia nyingi kufunga mabao. Tunatakiwa kucheza kwa tahadhari na kugeuza kila nafasi tunayoipata kuufungua mchezo.
“Tuko tayari tukitegemea mechi ngumu kama ilivyo kwa mechi zote lakini jambo la msingi ni kwamba timu iko sawa kiakili kuhakikisha inapata ushindi. Kila timu inapocheza na Yanga inakuwa na hamasa na inataka kuhakikisha inapata ushindi,” alisema Gamondi.
Katika hatua nyingine, kocha huyo alisema kuwa anafurahishwa na viwango vya viungo wake Khalid Aucho na Stephane Aziz Ki.
“Kwangu mimi wanacheza vizuri. Labda unaweza kuwaona hawajacheza kwa ubora mara zote lakini kwangu mimi ni jambo la kawaida. Unaweza kuona wachezaji kama Lewandowski, Mbappe na Haaland hawawezi kuwa bora kila wakati.
“Aziz Ki na Aucho hawawezi kucheza kwa asilimia mia lakini ukiwa umecheza mpira utafahamu kwamba kuna wakati unapungua kidogo lakini ni wachezaji wenye mchango mkubwa kwa timu,” alisema Gamondi.