
Dar es Salaam. Maabara Kuu ya Hospitali ya Muhimbili imetunukiwa cheti cha ithibati ya ubora, kitakachodumu kwa miaka mingine mitano.
Faida za kupata ithibati hiyo zimeelezewa kwa undani, ikiwemo kuimarika kwa ubora wa huduma za vipimo.
Ithibati hiyo hutolewa na Bodi ya Ithibati ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADCAS). Mchakato wa kuandaa Maabara Kuu ya Hospitali ya Muhimbili ili ipate ithibati ya ubora ulianza mwaka 2009, na ilipata ithibati hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2014.
Akizungumza katika hafla ya kupokea ithibati hiyo leo, Ijumaa, Mei 2, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, ametaja faida za ithibati hiyo, akisisitiza kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa ubora wa huduma za maabara zinazotolewa kwa wagonjwa ndani na nje ya hospitali hiyo.
Jingine ni kupunguza gharama kwa wananchi kwa kuwapa fursa ya kufanya vipimo vya maabara hapa nchini badala ya nje, kwani maabara hiyo inafuata miongozo ya kimataifa na inatoa majibu yanayoaminika kimataifa.
“Kingine ni kutoa huduma za vipimo vya maabara kwa ajili ya tafiti mbalimbali, ikiwa ni pamoja na tafiti za NIMR (Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania), MUHAS (Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili), Ifakara, Wizara ya Afya, na watafiti binafsi,” amesema Profesa Janabi, ambaye pia ni mshauri wa Rais kuhusu masuala ya afya na tiba.
Aidha, mtaalamu huyo wa afya amesisitiza kuwa, kwa kuwa Maabara Kuu ya Hospitali ya Muhimbili imekuwa ikishiriki katika kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa vyuo na hospitali mbalimbali, uwepo wa ithibati hiyo unahakikisha ubora wa mafunzo yanayotolewa katika hospitali hiyo.
Vilevile, ithibati hiyo inawezesha Maabara Kuu ya Hospitali ya Muhimbili kuwa na umaarufu na kuaminika na hospitali na taasisi mbalimbali, hivyo kuwa chanzo cha fedha cha uhakika kwa hospitali. Hii itawawezesha kutoa huduma kwa wagonjwa wengine wasio na uwezo, wakiwemo wanaohitaji msamaha wa malipo.
Wito wa Profesa Janabi kwa wataalamu wa maabara ni kuendelea kufuata kanuni na taratibu za utoaji huduma, na wafanyakazi kujivunia uwepo wa ithibati hiyo kama alama ya ubora.
Aidha, kwa hospitali za umma na binafsi, ametoa wito wa kuziongezea nguvu kifedha, kwa rasilimali watu na vifaa, ili zipate ithibati ya kimataifa itakayosaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa.
Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi katika Hospitali ya Muhimbili, Dk Mbonea Yonazi, amesema kuwa cheti hicho ni matokeo ya juhudi za kufanya vyema katika mchakato wa kaguzi za SADCAS.
Dk Yonazi amefafanua kuwa, kwa kawaida, maabara hiyo hufanya vipimo 368, na hadi sasa wamefanikiwa kupata ithibati ya vipimo 64. Ameongeza kuwa, ifikapo Juni 2025, watakuwa katika mchakato wa kuongeza vipimo vingine 20.
Amesema kuwa, ukiwa na maabara iliyokaguliwa na kupata ithibati, majibu ya vipimo yatakayopatikana katika maabara hiyo yatakuwa na hadhi ya kimataifa, na hivyo majibu yatakuwa sahihi na ya kuaminika kokote duniani katika maabara nyingine zilizopata ithibati.
Dk Yonazi amesema kuwa Hospitali ya Muhimbili, ambayo kwa siku huhudumia wagonjwa 4,000, inapokea sampuli takribani 3,500 kwa upande wa maabara kila siku.
Hata hivyo, uwezo wa maabara hiyo kuchakata sampuli ni 2,500 kwa saa moja, hivyo bado inafanya kazi kwa uwezo wa asilimia 60.